Home Kitaifa RAIS SAMIA MGENI RASMI TUZO YA MLIPAKODI BORA JANUARY 23.2025

RAIS SAMIA MGENI RASMI TUZO YA MLIPAKODI BORA JANUARY 23.2025

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatarajia kufanya maadhimisho ya siku ya shukrani na kutoa tuzo kwa Walipakodi bora kwa mwaka 2023/2024 tukio litakalofanyika Jijini Dar es Salaam January 23.2025.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Arusha Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano Bw. Richard Kayombo amesema mgeni rasmi katika maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan.

Amesema TRA imekuwa na utamaduni wa kuwashukuru na kuwapongeza walipakodi na wadau wao kutokana na mchango wao mkubwa wa kulipa kodi au kurahisisha ulipaji wa kodi.

Bw. Kayombo amesema lengo la kutoa tuzo hizo ni kutambua juhudi za walipakodi na kuunga mkono taasisi/watu binafsi waliowezesha TRA kukusanya kodi kwa urahisi.

Amesema Walipakodi watakaotunukiwa ni wale walioonesha mwitikio wa hali ya juu kwa hiari, mchango mkubwa katika ukusanyaji wa mapato, na wasio na rekodi yoyote ya udanganyifu au ukwepaji wa kodi katika kipindi husika.

TRA inashirikiana kwa karibu na wadau mbalimbali kufanikisha malengo yake, na kwa sababu hiyo, wadau wenye kiwango cha juu zaidi cha ushirikiano watapewa tuzo pia” amesema Kayombo.

Mwaka huu, jumla ya walipakodi na wadau 1228 watatunukiwa vikombe, ngao, na vyeti kama ishara ya kutambua mchango wao katika kujenga taifa kupitia ulipaji wa kodi kwa hiari au kwa kusaidia TRA kwa njia moja au nyingine katika ukusanyaji wa mapato” amesema Kayombo.

Ametaja vigezo vilivyozingatiwa katika utoaji wa tuzo hizo kuwa ni pamoja na Uzingatiaji wa sheria za kodi kwa hiari, Kulipa kiasi kikubwa cha Kodi au Ushuru kwa mwaka wa fedha 2023/24, Ulipaji kodi kwa hiari katika kipindi cha mwaka husika 2023/2024.

Vigezo vingine ni Uzingatiaji wa matumizi ya mashine za VFD/EFD kwa usahihi, Kuwasilisha ritani za kodi au nyaraka za forodha kwa wakati na kwa usahihi, Kulipa kodi na ushuru wa forodha kwa wakati na kwa usahihi, Kutohusika katika ukwepaji wa kodi na shughuli za udanganyifu.

Kayombo ameongeza vigezo vingine kuwa ni Kutoa ushirikiano kwa TRA katika masuala ya kikodi pindi inapohitajika na Kuboresha kiwango cha utendaji kazi katika maeneo yote ya uendeshaji.

Walipakodi waliotimiza vigezo vilivyotajwa watazingatiwa, mradi kwamba walipakodi hao hawajajihusisha na udanganyifu au ukwepaji wa kodi katika kipindi husika” amesema Kayombo.

Aidha amesema kutakuwepo na vipengele vya washindi wa kitaifa kwa
Walipakodi waliofuata sheria za kodi kwa hiari,
Walipakodi waliolipa kiasi cha kodi kikubwa kwenye ngazi ya wilaya au mkoa au kitaifa na
Walipakodi waliowasilisha nyaraka sahihi za forodha na kwa wakati.

Kayombo ametoa wito kwa walipakodi wote kuendelea kulipa kodi stahiki na kwa wakati na kuwahimiza wafanyabiashara wote kuendelea kutimiza wajibu wao wa kutoa risiti halali kila wanapouza, na wananchi kuhakikisha wanadai risiti za EFD, kwani hiyo ndiyo njia pekee takayounganisha watanzania wote kulipa kodi ya Serikali.

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!