Home Biashara RAIS SAMIA KUZINDUA MPANGO WA UTOAJI RUZUKU YA MBOLEA KWA WAKULIMA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MPANGO WA UTOAJI RUZUKU YA MBOLEA KWA WAKULIMA.

Na, Oscar Kasubi.

Kutokana na kupanda kwa bei za mbolea katika soko la Dunia na hapa nchini, Serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 150 kugharamia ruzuku ya mbolea itakayotolewa kwa wakulima wote nchini.

Akizungumza na waandishi wa Habari Jijini Dar es salaam leo tarehe 26,Julai 2022, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania, Dkt.Stephan Ngailo,amesema lengo ni kupunguza makali ya bei ya mbolea, kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza upatikanaji wa malighafi za viwanda vya ndani.

Pia Dkt.Ngailo amesema utoaji wa ruzuku utazingatia mahitaji halisi ya mkulima kulingana na taarifa za usajili na bajeti ya Serikali iliyotengwa, mbolea zitakozohusika kwenye ruzuku ni (DAP) mbolea kwa ajili ya kupandia na(UREA) kwa ajili ya kukuzia,ambazo ni takribani 50% ya matumizi ya mbolea yote nchini.

“Mbolea za kupandia na kukuzia za aina nyingine zitahusishwa kwenye ruzuku kulingana na mahitaji ya solo na mbolea zinazozalishwa na viwanda vya ndani zitaingia kwenye mpango wa ruzuku kulingana na mahitaji ya soko” amesema Dkt.Ngailo.

Katika kutekeleza mpango huo wa ruzuku na kwa kuzingatia uzoefu wa uliopatikana kutoka na mipango ya ruzuku katika miaka iliyopita, Serikali imeamua kutumia mfumo wa kidijitali katika kutekeleza mpango huo katika mwaka wa fedha wa 2022 /2023, kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utoaji ruzuku kupunguza mianya ya udanganyifu, muda na gharama ya usimamizi.

Katika kudhibiti udanganyifu Dkt.Ngailo amesema mfumo huo utatumia mfumo maalum wa kidigitali kuratibu shughuli zote na kwamba Makampuni yataingiza au yatazalisha mbolea Nchini na kuifungasha kwanye mifuko yenye uzito wa kilo 25 na 50, ambayo itaandikwa ‘Mbolea ya Ruzuku’ na itachapwa alama maalum (QR code) itakayotolewa na Mamlaka yaani TFRA.

Akielezea namna mkulima atavyopata mbolea yake ya ruzuku Mkurugenzi huyo amesema, mkulima aliyesajiliwa ataenda kwa mfanyabiashara wa Mbolea aliyesajiliwa kwa ajili ya kununua mbolea na kuonyesha namba ya utambulisho aliyopewa wakati wa usajili na mkulima at afanya malipo kwa mfanyabiashara kwa bei elekezi ya ruzuku iliyoweka.

“Waziri wa kilimo Mhe. Hussein Bashe alizindua mwongozo wa utekelezaji wa Mpango wa ruzuku pamoja na usajili wa wakulima tarehe, 4 Julai, 2022 Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma hii ilikuwa moja ya hatua muhimu ya kufanikisha mpango huu” amesema Dkt.Ngailo.

Katika hatua nyingine Dkt.Ngailo alifahamisha kuwa mpango huo wa utoaji ruzuku ya mbolea kwa wakulima sasa utazinduliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, siku ya kilele cha maonyesho ya wakulima maarufu kama Nanenane yatakayofanyika kitaifa Mkoani Mbeya tarehe 8.8.2022.

MWISHO.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!