Home Kitaifa RAIS SAMIA ARUDISHA MATUMAINI MBARALI

RAIS SAMIA ARUDISHA MATUMAINI MBARALI

Makamu Mwenyekti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara Abdulrahaman Kinana amewaambia wananchi wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amekubali ombi lao la kuendelea na shughuli za kilimo katika eneo lililozuiwa kupitia tangazo la Serikali la GN 28, kama ilivyokubaliwa mwaka jana.

Tangu kutolewa kwa katazo hilo, wananchi wamekuwa wakilalamika kuwa mchakato wa kufikia maamuzi hayo haukuwa shirikishi na kuiomba serikali kuliondoa katazo hilo ambalo linaathiri ustawi wa maisha yao na kipato.

Akizungumza wakati akihitimisha kampeni za CCM katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mbarali mkoani Mbeya, zilizofanyika katika Kijiji cha Chimala, Makamu Mwenyekiti Kinana alisema mgombea Ubunge wa CCM Bahati Ndingo, Madiwani wa CCM, Viongozi wa CCM na wananchi walimueleza amuombe Rais Samia waendelee kulima wakati suala hilo linazungumzwa.

Nimemueleza Rais jana kuwa wananchi wa Mbarali wanaomba waendelee kulima kwa sababu msimu unaanza mwezi ujao (Oktoba) na Rais akasema sawa waendelee, kwa yale maeneo yote yaliyoruhusiwa mwaka jana Rais amekubali mwendelee kulima,” alisema.

Akizungumzia ombi la mgombea ubunge kuhusu ujenzi wa barabara iliyokaa muda mrefu kutoka Lujewa, Madibila hadi Mafinga, Kinana alisema atawasiliana na wahusika (Waziri wa Ujenzi) ili ujenzi wa barabara hiyo uanze kama ilivyoahidiwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Awali wakati akiomba kura Bahati Ndingo Mgombea Ubunge wa CCM Jimbo la Mbarali, alitumia nafasi hiyo kuelezea masuala mbalimbali yanayoendelea katika wilaya hiyo yakiwemo maendeleo makubwa ambayo yamefanywa na serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia.

Bahati alikiiomba Chama na serikali kuangalia upya changamoto ya migogoro ya ardhi iliyopo ndani ya wilaya hiyo. Alisema asilimia zaidi ya 90 ya wananchi wa Wilaya ya Mbarali ni wakulima, hivyo ardhi ndio maisha yao na ndio uchumi wao.

Uchaguzi huo unafanyika baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Francis Mtega kufariki dunia Julai Mosi mwaka huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!