Home Kitaifa RAIS SAMIA AMEDHAMIRIA KUENDELEA KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA-MAJALIWA

RAIS SAMIA AMEDHAMIRIA KUENDELEA KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma za afya kwa kuwezesha upatikanaji wa wataalam, dawa, vitendanishi na vifaa tiba.

Mheshimiwa Majaliwa ametoa kauli hiyo leo Oktoba 26, 2022 baada ya kushuhudia utiaji saini wa Makubaliano ya Ushirikiano baina ya Bohari ya Dawa Tanzania (MSD) na Serikali ya Jimbo la Chungcheongbuck nchini Korea kusini.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa  leo Oktoba 26, 2022 ameshuhudia  utiaji saini wa makubaliano  ya Ushirikiano baina ya Bohari ya Dawa Tanzania (MSD na Seikali ya Jimbo la Chungcheongbuck nchini Korea . Pichani,   Mtendaji Mkuu wa MSD, Tukai Lavere (wa pili kushoto) na Gavana wa Jimbo hilo Kim Young Hwan (wa pili kulia) wakitia saini makubaliano hayo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Akizungumza wakati wa tukio hilo, ambalo pia lilihudhuriwa na Gavana wa jimbo la Chungcheongbuck, Mheshimiwa Majaliwa amesema “Tukio hili la utiaji saini wa makubaliano haya ni ishara kwamba sasa tunakwenda kuimarika kwenye sekta ya dawa, mkataba huu kwetu ni muhimu kwa kuwa tunahitaji kujiimarisha katika eneo la upatikanaji wa dawa na tafiti.”

Sehemu ya makubaliano katika mkataba huo ni kujadili na kuendeleza mahusiano ya kibiashara katika nyanja za masoko ya bidhaa zinazozalishwa na Makampuni ya dawa katika jimbo hilo.

Maeneo mengine ni kubadilishana watumishi, semina za pamoja za wataalamu wao katika nyanja mbalimbali, kubadilishana na kupeana taarifa za uwekezaji kwenye sekta ya dawa, msaada wa kitaalamu na wataalam.

Mheshimiwa Majaliwa alimueleza Gavana huyo kuwa, kutokana na mpango wa Serikali wa kuendelea kuimarisha eneo la utoaji huduma za afya, Serikali ya Tanzania inawakaribisha wawekezaji kwa ajili ya kujenga viwanda vya dawa na vifaa tiba ili kuwezesha upatikanaji rahisi wa dawa na vifaa tiba.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!