Na Benny Mwaipaja, Kigamboni
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam, Bi. Halima Bulembo na viongozi wenzake kwa kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazoikabili jamii katika Wilaya hiyo kwa vitendo.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa pongezi hizo leo alipompigia simu Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakati akihutubia Wakazi wa Kigamboni katika eneo la Mji Mwema, akimwakilisha Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, katika hafla ya kupokea na kukabidhi vifaa mbalimbali kwa makundi maalum katika Wilaya ya Kigamboni.
Akizungumza kwa njia hiyo ya simu huku akishangiliwa na Wakazi wa Kigamboni waliohudhuria hafla hiyo iliyobeba kaulimbiu ya “Kigamboni Salama na Mama Samia”, alisema kuwa ameguswa na hatua ya uongozi wa Wilaya hiyo kuwatembelea wananchi mahali waliko, kuwasikiliza na kutatua shida zao.
“Nimeambiwa kwamba hapo mtatoa majiko yanayotumia gesi kwa akina mama na baba lishe, vitimwendo kwa watu wenye ulemavu, vifaa vya kujifungulia kwa akina mama, mavazi ya kuwatambulisha waendesha pikipiki bodaboda (reflactors), na vituo vya kujikinga na jua pamoja na mvua kwa ajili ya waendesha bodaboda, nimefurahishwa na hatua hiyo na ninawapongeza sana” alisema Mhe. Rais Dkt. Samia.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) alitoa pia pongezi kwa Uongozi wa Wilaya ya Kigamboni kwa kubeba kwa vitendo ajenda za Rais wa Nchi, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyedhamiria kwa dhati kuwahudumia wananchi ili wafikie maendeleo.
Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa, kupitia kwa Dkt. Nchemba aliwataka Viongozi wa Mikoa na Wilaya kote nchini, kuiga mfano wa mipango na mikakati ya Wilaya ya Kigamboni, ya kuwatembelea wananchi katika maeneo yao na kutatua shida zao badala ya kusubiri wananchi washike mabango ya malalamiko na wanapotembelewa na Viongozi Wakuu wa Nchi.
Akielezea namna Serikali ilivyojipambanua kuleta maendeleo ya wananchi kwa haraka, Dkt. Nchemba alisema katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, maendeleo makubwa yameshuhudiwa ikiwemo kuimarika kwa huduma za jamii kama vile elimu, afya, maji, kilimo, mifugo, miundombinu ya barabara na mambo mengine kadha wa kadha.
Dkt. Nchemba, alifafanua kuwa Serikali imeongeza bajeti kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta zote nchini ambapo kiwango cha fedha hizo hakijawahi kuwa kikubwa kama ilivyo sasa katika kipindi chochote kilichopita.
Alitolea mfano fedha za Mfuko wa Barabara Vijijini-TARURA, ambapo alisema bajeti imeongezwa kutoka shilingi bilioni 200 kwa mwaka hadi kufikia zaidi ya shilingi trilioni 1.3, na mikopo ya elimu ya juu kutoka shilingi bilioni 400 hadi kufikia shilingi trilioni 1.
Aidha, aliwaagiza watumishi wa umma, kuwahudumia wananchi kwa upendo katika maeneo yao ya kazi ili kuondoa manung’uniko kutoka kwa jamii.
“Wadau wa Sekta binafsi endeleeni kujitokeza ili kuiunga mkono Serikali ya awamu ya sita katika kutekeleza mipango, mikakati pamoja na afua za kuinua ustawi wa jamii ya Watanzania” Alisema Dkt. Nchemba.
Aidha, aliwataka Watumishi wanaosimamia miradi katika halmashauri zote wazingatie ubora wa miradi inayotekelezwa ili iwiane na thamani halisi ya fedha inayotolewa na Serikali kwa kuwa fedha hizo ni kodi ya wananchi, hivyo wahakikishe wananchi wanafaidika kutoka na huduma zinazotolewa kupitia kodi zao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Bi. Halima Bulembo, alisema kuwa Uongozi wa Wilaya hiyo umetembelea kata zote za Wilaya hiyo na kusikiliza kero na mahitaji ya wananchi na kuja na mpango na mikakati ya ndani ya kutatua changamoto hizo.
Alisema kuwa makundi mbalimbali ya kijamii yalifikiwa katika maeneo husika ambapo ilibainika kuwa wakina baba, wanawake, vijana, na makundi maalumu yanauhitaji mkubwa wa mitaji, miundombinu ya kufanyia biashara pamoja na zana zinazoweza kuwarahisishia maisha.
Bi. Bulembo alisema kuwa walibaini uwepo wa vijana zaidi ya 5,470 waliojiajiri katika sekta ya usafirishaji abiria kwa njia ya bodaboda, akina baba na mamalishe zaidi ya 2,000, wazee 4895 na watu wenye ulemavu 789 wametambuliwa, ambao kwa pamoja wilaya imekuja na mpango wa kutatua kero zao kupitia kampeni ya Kigamboni Salama na Mama Samia.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kigamboni, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile, aliiomba Serikali kuifanya Kigamboni kuwa kama Dubai au Guangzhou ya China, kwa kujenga miundombinu ya kuvutia uwekezaji wa viwanda na biashara, lakini pia kwa kujenga miundombinu ya barabara.
Alieleza kuwa wawekezaji wengi wameonesha nia ya kuwekeza katika Wilaya ya Kigamboni lakini baadhi yao wanakwazwa na miundombinu ya barabara na kwamba Serikali ikitatua changamoto hizo, eneo hilo litakuwa kitovu cha biashara na mapato ya Serikali na hatimaye kuboreshwa kwa maisha ya watu.
Mwisho