Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewasili na kupokelewa na Viongozi mbalimbali pamoja na wananchi kwenye uwanja wa ndege wa Dodoma akiwa na Tuzo Maalum ya Kimataifa ya The Global Goalkeeper Award.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepokea tuzo ya kimataifa ya Global Goalkeeper Award kutoka Taasisi ya Bill & Melinda Gates Foundation, ikiwa ni sehemu ya kutambua juhudi zake katika kuimarisha sekta ya afya nchini Tanzania. Tuzo hiyo ilitolewa katika hafla maalum iliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Sharifa B. Nyanga, tuzo hiyo, ambayo hutolewa kwa viongozi waliotoa mchango mkubwa katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), ilikabidhiwa kwa Rais Samia na Dkt. Anita Zaidi, Rais wa Kitengo cha Usawa wa Kijinsia wa Taasisi ya Gates.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Rais Samia alisema kuwa kati ya mwaka 2020 hadi 2024, serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya afya, jambo lililowezesha kuongezeka kwa vituo vya kutolea huduma za dharura za afya ya mama na mtoto kutoka 340 hadi 523. Aidha, idadi ya wataalamu bingwa wa afya ya mama na mtoto imeongezeka kutoka 69 hadi 308, huku mashine za ultrasound na sonography zikiongezeka kutoka 345 hadi 970.
Rais Dkt. Samia alisisitiza kuwa serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika kuimarisha lishe bora ili kutokomeza changamoto za utapiamlo na udumavu kwa watoto nchini. “Tuzo hii si yangu peke yangu, bali ni ya watumishi wote wa sekta ya afya ambao ujuzi na ustahimilivu wao umewezesha nchi yetu kupata mafanikio haya,” alisema Rais Samia.
Tuzo ya Global Goalkeeper hutolewa kila mwaka kwa viongozi na taasisi zinazochangia kwa kiasi kikubwa katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu duniani, hususan katika kuboresha maisha ya watu kupitia sekta muhimu kama afya, elimu, na usawa wa kijinsia.