Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar,
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi amekitaka Kigoda cha taaluma cha Sheikh Abeid Amani Karume kutilia mkazo zaidi masuala ya kufanya tafiti mbalimbali kwa ajili ya maendeleo nchini.
Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo alipozindua rasmi Kigoda cha taaluma cha Sheikh Abeid Amani Karume katika ukumbi wa Dkt.Ali Mohamed Shein, Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja tarehe 15 Juni 2024.
Aidha Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa Serikali itafanya juhudi za kuhakikisha malengo ya Kigoda hicho yanafanikiwa ili kuleta tija za kihistoria, kitaaluma na kimaendeleo kwa ustawi wa jamii.
Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi amesema Kigoda hicho kiwe ni jukwaa ambalo litaendeleza na kutunza tunu za taifa za Mapinduzi na Muungano ambazo zimetimiza miaka sitini.
Kwa upande mwingine Rais Dkt.Mwinyi amempongeza Profesa Egiland Pius Mihanjo kwa kuwa Mwenyekiti wa kwanza wa Kigoda hicho.
Viongozi mbalimbali wa Serikali, Vyama vya siasa, Vyombo vya ulinzi na usalama wameshiriki wakiwemo Rais Mstaafu wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete, Marais wastaafu wa Zanzibar Dkt. Amani Abeid Karume na Dkt.Ali Mohamed Shein , na Mwanasiasa Mkongwe Mzee Stephen Wassira.