Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewahimiza Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kuendelea kufanya utafiti wenye lengo la kupata ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili jamii ya Zanzibar na kutoa ushauri wa kitalaamu.
Rais Dkt. Mwinyi amesema hayo katika Mahafali ya Kumi na Tisa (19) ya Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) ukumbi wa Dkt.Mohamed Ali Shein Kampasi ya Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja tarehe: 28 Disemba 2023.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar zimejiandaa kuhakikisha vijana wote wenye sifa za kujiunga na Vyuo vikuu wanapatiwa mikopo ili kuwawezesha kuendelea na masomo yao.
Kwa upande mwingine Rais Dkt. Mwinyi amewapongeza wahitimu Wanawake kwa kushika nafasi za juu na kufikia asilimia hamsini na nane (58) kati ya wahitimu 2,102 wa Chuo hicho.
Pia katika mahafali hayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametunukiwa Shahada ya Uzamivu ya Heshima katika fani ya Usimamizi wa Utalii na Masoko ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).