Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali imedhamiria kujenga uwanja mpya mwingine wa kisasa ambao utatumika katika mashindano ya AFCON mwaka 2027.
Rais Dk.Mwinyi amesema hayo akizindua rasmi Uwanja mpya wa Amaan Complex tarehe:27 Desemba 2023, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha, Rais Dk.Mwinyi ameeleza kuwa Serikali imelenga kujenga miundombinu ya michezo kila wilaya kwa viwanja vipya vya kisasa.
Vilevile Rais Dk.Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Ujerumani kupitia shirika la maendeleo GIZ imefunga mkataba wa makubaliano kwa ajili ya ujenzi wa viwanja vitano vya michezo midogomidogo ikiwemo mpira wa kikapu, mpira wa wavu , mpira wa mikono na mpira wa pete.
Viwanja hivyo vinatarajiwa kujengwa Kangani Wilaya ya Mkoani, Mchangamdogo Wilaya ya Wete, Tumbatu na Mkokotoni Wilaya ya Kaskazini A na Haile Selasie Wilaya ya Mjini pamoja na viwanja vitatu vya Tennis Chakechake, Chuo kikuu cha SUZA Kampasi ya Nkurumah na Skuli ya Regeza Mwendo katika Wilaya ya Magharibi B.
Halikadhalika Serikali imefanikiwa kuwapeleka vijana katika nchi mbalimbali ikiwemo Uturuki na Afrika Kusini kwa lengo la kuendelezwa na baadae kucheza soka la kulipwa.
Rais Dk.Mwinyi amewahimiza wananchi kushiriki Tamasha la kila mwaka la mazoezi linalofanyika tarehe Mosi ya mwaka mpya.