Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi ametaja baadhi ya mambo aliyojifunza kutoka kwa Hayati Mzee Mwinyi wakati wa uhai wake.
Hayati Mzee Mwinyi alikuwa na Subira kubwa wakati alipokuwa kiongozi hususan kipindi cha mageuzi ya Kisiasa na Kiuchumi.  Watu walimsema vibaya kwa mambo ya kutunga katika vyombo vya Habari lakini hakuwahi kumjibu  yeyote kwa mabaya waliyomsema.
Alhaj. Dk. Mwinyi amesema yeye amejifunza kusubiri kwa fundisho alilolipata kwa Mzee wake kwa kumpa mafunzo mema.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi amesema wakati Marehemu baba yake alipokuwa akitibiwa Uingereza aliwataka madaktari na familia arudishwe nyumbani na baadae apelekwe Zanzibar, maneno hayo aliyarudiarudia hata baada ya kufika Dar es Salaam.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo katika Dua ya khitma iliyoandaliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya kumuombea aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Marehemu Mzee Ali Hassan Mwinyi ambayo imefanyika leo tarehe: 05 Machi 2024, Msikiti wa Zinjibar Mazizini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
Rais Dk. Mwinyi ameishukuru kamati ya Kitaifa ya Maandalizi ya Mazishi inayoongozwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla pamoja na wajumbe wake.