MKOA wa Pwani umepatiwa Wauguzi 120 ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa kada hiyo.
Hayo yamesemwa mjini Kibaha na Katibu Tawala Mipango na Uratibu wa Mkoa wa Pwani Edina Kataraiya ambaye alimwakilisha Naibu Waziri wa Afya Dk Godwin Mollel wakati wa Maadhimisho siku ya Uuguzi kimkoa.
Kataraiya amesema kuwa serikali imeendelea kutatua changamoto mbalimbali za huduma za afya ikiwa ni pamoja na kuongeza wahudumu wa afya ili kuboresha utoaji huduma.
“Kada ya uuguzi ni uti wa mgongo wa huduma za afya ndiyo sababu serikali inaboresha kwani bila ya wauguzi hakuna huduma hizo hivyo toeni huduma kama kiapo chenu kinavyosema upendo, utu na uadilifu,”amesema Kataraiya.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA) Steven Brown amesema kuwa katika Muundo wa Utumishi wa Kada ya Uuguzi na Ukunga ambacho kinamtaka Ofisa Muuguzi kabla hajafikia Kiwango cha mwisho cha Mshahara wake yaani TGHSG awe na Masters ambacho ni kikwazo kwa wauguzi.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani Kusirye Ukio amesema kuwa huduma wanayotoa wauguzi ni ibada na Hospitali ni madhabahu hivyo waendelee kudumisha ibada zao.