Home Kitaifa “PROGRAMU YA MAENDELEO YA SEKTA YA MAJI AWAMU YA TATU NI SHIRIKISHI”-WAZIRI...

“PROGRAMU YA MAENDELEO YA SEKTA YA MAJI AWAMU YA TATU NI SHIRIKISHI”-WAZIRI AWESO.

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amezindua rasmi awamu ya Tatu ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji iliyoanza Julai 2022 hadi Juni 2026.

Uzinduzi huo umefanyika leo jijini Dodoma na kuhudhuriwa wawakilishi kutoka sekta mbalimbali zinazoshughulika na huduma ya maji ambapo amesema programu hiyo ni shirikishi ili kuleta matokeo kwa wananchi.

Waziri Aweso amesema gharama ya utekelezaji wa Programu hiyo inakadiriwa kuwa Dola za Marekani Bilioni 6.46 na inalenga kufanikisha utekelezaji wa miradi ya usimamizi na uendelezaji rasilimali za maji, upatikanaji wa majisafi na salama na miradi ya usafi wa mazingira hapa nchini.

Aidha, amezitaka Asasi za Kiraia (AZAKI) na wadau wote wa Sekta ya Maji kuendelea kushirikiana na Sekta ya Maji ambayo ni muhimu katika kuinua uchumi wa jamii hapa nchini.

“Nawashukuru sana kwa kujitokeza kwa sababu uwepo wenu katika hafla hii kunaonyesha dhamira yenu ya dhati ya kuendelea kushirikiana na Sekta ya Maji katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi, salama na ya uhakika. Niwaombe tuendeleze ushirikiano huu ili tuyafikie kwa pamoja malengo tuliyojiwekea” Waziri Aweso amesema.

Amefafanua kuwa baada ya kukamilika kwa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji Awamu ya Kwanza na ya Pili, Wizara inajivunia mafanikio makubwa katika Sekta ya Maji ikiwa ni pamoja na maboresho katika usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji ikiwemo kuanzishwa kwa Bodi tisa za Maji za Mabonde, maabara 7 kati ya 17 za Ubora wa Maji kupewa vyeti vya Ithibati, kuimarika kwa kiwango cha huduma ya maji vijijini hadi kufikia asilimia 72.3.

Kwa upande wake mwakilishi wa Wadau wa Maendeleo Bi. Ruth Kennedy Walker kutoka Benki ya Dunia ameipongeza serikali kwa jitihada zinazofanyika kuhakikisha changamoto za upatikanaji wa majisafi na salama zinapatiwa ufumbuzi. Amesema Benki ya Dunia iko tayari kuendeleza ushirikiano huo.

Aidha, mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Saitore Laizer amesema program hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza magonjwa ya mlipuko, kuongeza usafi katika maeneo ya umma na kuimarisha afya ya Watanzania.

Amesema kiwango cha huduma ya maji katika maeneo ya huduma ya afya kimeimarika hivyo huduma za afya kuwa bora na salama

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!