Programu ya Stawishi Maisha, inayosimamiwa na Serikali ya Tanzania kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa kushirikiana na UNICEF, imezinduliwa rasmi katika Kijiji cha Mkiu, Kata ya Mkamba, Wilaya ya Mkuranga .
Programu hii inalenga kuboresha lishe kwa watoto wa umri wa miezi 0 hadi miaka 5, mama wajawazito, na mabinti balehe kwa kuwapatia elimu ya lishe bora kupitia vipindi vya redio.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Shedrack Mziray, alieleza mradi huu ni sehemu ya jitihada za TASAF kupambana na utapiamlo katika kaya zilizo kwenye mpango huo.
“Kupitia mpango huu, tunalenga kukuza maendeleo ya rasilimali watu na kuwezesha kaya kujikwamua kutoka kwenye mnyororo wa umaskini kupitia elimu ya lishe bora,” alieleza Mziray.
Kadhalika Mziray aliongeza kuwa ,usambazaji wa redio zinazotumia nishati ya jua utachangia kuwafikia wanajamii wengi, kuwapa nafasi ya kushiriki mijadala kuhusu lishe bora, pamoja na elimu na burudani, kwa kipindi cha miezi sita.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, ambaye pia ni Katibu Tawala wa Wilaya, Omary Mwanga aliishukuru TASAF na wadau wa maendeleo, UNICEF, kwa mchango wao muhimu katika mpango huu wa lishe bora.
Aliwahimiza wananchi wa Mkuranga kushiriki kikamilifu ili kuleta matokeo chanya na kuwekeza katika lishe bora ili kuepuka udumavu.
“Tunahimiza jamii kuwekeza katika lishe bora, kwani serikali imefanya uwekezaji mkubwa, na tunapaswa kuuthamini,” alisema Katibu Tawala.
Kwa upande wake, Mratibu wa TASAF Mkoa wa Pwani, Roseline Kimaro, kwa niaba ya viongozi wa mkoa wa Pwani, aliishukuru serikali kwa kuendelea kuimarisha uchumi wa kaya za wanufaika wa mpango wa TASAF kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kama UNICEF.
Alieleza, Mkoa wa Pwani unatekeleza mipango na mikakati iliyowekwa na serikali kuhakikisha lishe inaboreshwa na kupunguza utapiamlo kwa watoto.
“Utekelezaji wa programu hii ya Stawishi Maisha katika mkoa huo, itasaidia kuimarisha mipango ya mkoa ya kuhakikisha wananchi wanapata lishe bora” alisema Roseline.
Wilaya ya Mkuranga ni miongoni mwa halmashauri 18 zinazotekeleza mpango huu wa majaribio, ambapo vikundi 30 vimeundwa katika kata 13 na vijiji 19.
Katika utekelezaji huo ,vikundi hivyo vitakutana mara moja kwa wiki kusikiliza vipindi vya redio vinavyoelimisha na kuhamasisha umuhimu wa lishe bora, kupitia redio zinazotumia nishati ya jua walizopewa.