Home Afya PROF. MUHONGO: YAMETIMIA HOSPITALI YA MUSOMA VIJIJINI YAANZA KUTOA HUDUMA

PROF. MUHONGO: YAMETIMIA HOSPITALI YA MUSOMA VIJIJINI YAANZA KUTOA HUDUMA

Na Shomari Binda-Musoma

MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini, Profesa Sospeter Muhongo amesema hatimaye imetimia hodpitali yenye hadhi ya wilaya kuanza kutoa huduma za afya kwenye jimbo hilo.

Kauli hiyo ameitoa mara baada ya kufanyika kwa uzinduzi wa utoaji huduma ulifanywa na mkuu wa wilaya ya Musoma Dkt. Khalfan Haule.

Akizungumza mbele ya wananchi walioshuhudia uzinduzi huo,Muhongo amesema viongozi na wananchi wa Musoma vijijini wanaishukuru serikali kwa ujenzi wa hospital hiyo na sasa imeanza kutoa huduma.

Amesema kila ambacho wamekuwa wakiiomba serikali katika utoaji wa huduma za kijamii wamekuwa wakiwapatia na sasa wamepata hospital yenye hadhi ya wilaya.

Muhongo amesema yapo mapungufu ambayo ameyasikia lakini hakuna budi kuishukuru serikali kwa ujenzi wa hospital hiyo.

“Kwanza tujipongeze kwa hili na kuishukuru serikali kwa kuwa kila tunachokiomba mgao ukija tunapata hili ni jambo la kuishukuru serikali yetu”

“Ni matumaini yetu kwa yale mapungufu yaliyojitokeza yatakwenda kukamilishwa na serikali na kupata huduma bora za afya” amesema Muhongo.

Mkuu wa wilaya ya Musoma,Dk.Khalfan Haule,amesema wataalam wameshafika tayari kwa kuanza kutoa huduma za afya kwa wananchi wa Musoma vijijini.

Amesema hospitali imejengwa katikati ya halmashauri kwenye Kitongoji cha Kwikonero, Kijiji cha Suguti, Kata ya Suguti.

Haule amedai hospitali itakuwa ikitoa huduma za afya kwa kiwango cha hadhi ya hospitali ya Wilaya na hadi sasa serikali imeishatoa shilingi bilioni 3.49 kwa ajili ya ujenzi, na shilingi milioni 600 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na dawa.

Amesema majengo muhimu tisa (9) yamekamilika, na majengo mengine sita (6) yanaendelea kujengwa likiwemo jengo la kufulia (laundry)

Mkuu huyo wa wilaya amesema hospitali ina vifaa vya kisasa, vikimemo: Digital X-ray, Ultrasound na mitambo ya kutengeneza Oxygen ambayo inapelekwa sehemu ya matibabu kupitia mtandao wa paipu.

Aidha amesema mitungi ya Oxygen ipo ikiwa ni kwa matumizi ya dharura au kusaidia mahitaji ya hospitali nyingine, vituo vya afya na zahanati.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!