Na Shomari Binda-Dodoma
MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini Prof. Sospeter Muhongo amesema kupatikana kwa umeme wa uhakika kutachochea kwa kasi ukuaji wa uchumi.
Huo ulikuwa sehemu ya mchango wake wakati akichangia hii leo bungeni mjadala kuhusu hali ya uchumi na mpango wa maendeleo ikiwemo bajeti ya 2023/2024.
Amesema umuhimu wa uchumi kukua kwa zaidi ya asilimia 8 kwa mwaka (8-10% growth) umeme mwingi, wa uhakika na wa bei nafuu unahitajika.
Muhongo amesema umeme kwa sasa bado haujatosha ambapo megawati 10000 zinahitajika ili kufikia kiwango cha uhitaji.
Amesema Tanzania inahitaji umeme mwingi wa uhakiki ikiwa ni pamoja na vyanzo vingi vya upatikanaji wake.
Katika mchango wake huo,Muhongo pia amependekeza kupunguzwa kwa bei ya umeme ili kuweza kuwapata watumiaji wengi.
Mbunge huyo amesema kitu kingine kitakachopelekea uchumi kukua kwa kasi ni pamoja na uchumi wa gesi ukitumiwa vizuri.
“Kingine kitakachofanya uchumi ukue kwa kasi na umasikini kutokomea ni lazima tuwekeze kwenye gesi na mafuta na hapo ndio tutaweza kufikia malengo” amesema Muhongo.
Amesema anaiunga mkono hoja kwa kuwa Musoma vijijini ipo miradi ambayo inakwenda kuanza mwezi wa 8 ikiwemo ya barabara na kilimo cha umwagiliaji ambayo itakwenda kuinua uchumi wa wananchi.