Na Shomari Binda-Musoma
MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini Profesa Sospeter Muhongo amezitembelea familia za kaya 15 zilizoathirika na mvua Kata ya Etaro.
Familia zilizoathirika zaidi kwa mvua hizo kubwa zilizonyesha mfululizo zinatoka kwenye vijiji vya Busamba na Etaro na kuharibu makazi.
Licha kuharibu makazi mvua hizo zimepelekea kifo cha mtoto mchanga mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu ambaye aliangukiwa na ukuta.
Kwa sasa familia ambazo zimeathirika kutokana na mvua hizo zimehifadhiwa na majirani pamoja na ndugu huku tathimini zaidi za athari za mvua hizo zikifanyika.
Mbunge Profesa Muhongo ametembelea familia hizo na kutoa pole na rambirambi kwa familia iliyopotelewa na mtoto kwa kutoa fedha za kujikimu.
“Nimekuja kuwapa pole ndugu zangu kutokana na athari hizi za mvua ambazo mmezipata kwenye maeneo yenu.
“Nawaomba tuwe wastahimilivu katika kipindi hiki kigumu ambapo tathimini zaidi zikiendelea kufanyika ili kupata msaada zaidi”,amesema Muhongo.
Baadhi ya waathirika wa mvua hizo wamemshukuru mbunge huyo kwa kuwatembelea na kuwasaidia fedha kwaajili ya kujikimu.
Wamesema msaada huo umekuja wakati muafaka ili kuweza kuwasaidia katika kipindi hiki kigumu walichukuwa nacho kutokana na athari za mvua.