Mbunge wa Jimbo la Ubungo Prof. Kitila Mkumbo amesema Serikali inaendelea kufanya maboresho ya miundombinu ya barabara katika Jimbo la Ubungo ili kuhakikisha zinapitika kwa asilimia 90 ka kuwa na barabara za kiwango cha lami asilimia 50 ifikapo mwaka 2025.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa Jimbo la Ubungo Prof. Kitila amesema Jimbo hilo lina jumla ya Km 197 za barabara kati yake Km 168 zinasamiwa na TARURA huku Km 28 zikiwa chini ya usimamizi wa TANROAD.
Amesema wakati anaingia madarakani mwaka 2020/2021 kulikuwa na asilimia 20 ya barabara za lami lakini sasa hivi kuna jumla ya asilimia 28 huku ujenzi ukiendelea kwenye baadhi ya maeneo.
Amesema katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu wameweza kujenga barabara Km 34 kwa kiwango cha changarawe huku kwa mwaka wa fedha 2022/2023 wakitarajia kujenga barabara 31 kwa kiwango cha changarawe.
Kuhusu mradi wa DMDP amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia utekelezwe wilayani Ubungo na Kigamboni ambapo wilaya ya Ubungo itapatiwa Sh. Bilioni 96 zitakazojenga Km 42.7 za barabara kwa kiwango cha lami.
Kuhusu sekta ya Elimu Prof. Kitila amesema wilaya ya Ubungo ilinufaika na fedha za UVIKO 19 kwa kupatiwa Sh. Bilioni 3.2 zilizojenga vyumba 160 vya madarasa.
Prof. Kitila amesema ujenzi huo wa vyumba vya madarasa umesaidia kumaliza changamoto ya vyumba vya madarasa katika Jimbo la Ubungo.
Mbunge huyo pia amezungumzia suala la Bima ya Afya kwa wote ambayo itawanufaisha watanzania wite kwa kupatiwa huduma za matibabu bila ya kuwa na fedha mkononi hali itakayosaidia kuokoa maisha ya watanzania ambao walikuwa wakikosa matibabu kwa kukosa fedha za matibabu.
“Mwezi Novemba tunakwenda bungeni na miongoni mwa mambo tutakayofanya ni kupitisha sheria ya huduma ya Afya kwa wote” amesema Prof. Kitila
Aidha Prof. Kitila amesema Serikali inaendelea kujali maisha ya wananchi kutokana na kuwepo kwa uhusiano mkubwa baina ya siasa na hali za wananchi ndiyo maana Rais Samia Suluhu Hassan akaamua kutoa ruzuku katika mafuta ya Petrol ili kupunguza makali ya maisha.
Mwisho