Home Kitaifa Prof. KITILA AWATAKA VIJANA KUWAAMBIA UKWELI VIONGOZI WANAPOKOSEA BADALA YA KUWAPAMBA

Prof. KITILA AWATAKA VIJANA KUWAAMBIA UKWELI VIONGOZI WANAPOKOSEA BADALA YA KUWAPAMBA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji na Mbunge wa Jimbo la Ubungo (CCM) Prof. Kitila Mkumbo amewataka vijana kuacha kuwa ‘Machawa’ wa watu binafsi maana ni utumwa.

Akizungumza katika mkutano wa Umoja wa Vijana wa Tawi la Shule ya Sheria Prof. Kitila amesema vijana wanapaswa kuwa ‘Chawa’ /wafuasi wa Chama na misingi yake ili kuwavutia wenzao waliopo nje ya Chama.

Amesema vijana ndiyo tegemeo la Chama Cha Mapinduzi hivyo wanapaswa kuwa wafuasi wa misingi ya Chama na siyo watu binafsi hali itakayokitangaza zaidi na sera zake kwa wananchi.

“Ninyi vijana wa chuo ‘wasomi’ uchawa wenu lazima uwe wa tofauti kwa kuwa wafuasi wa misingi ya Chama ikiwemo Utu, Uhuru, Usawa, Fursa sawa kwa wote na kusaidia kupeana mawazo ya namna ya kutatua changamoto ya ajira nchini” Prof. Kitila Mkumbo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji na Mbunge wa Jimbo la Ubungo.

Prof. Kitila Mkumbo amesema mtu akiwa mfuasi ‘chawa’ wa mtu binafsi anakuwa mtumwa kwa mtu huyo na wala haimsaidii Kiongozi husika maana wanaishia kuwapamba badala ya kuwambia ukweli jambo ambalo siyo sawa.

“Mkiwa wafuasi wa Chama mtawasaidia Viongozi kwa kuwakosoa pale wanapokosea badala ya kuishia kuwapamba, Sisi enzi zetu tulikuwa wawazi kwa kuwaambia ukweli Viongozi wetu nanyi mnapaswa kuwa hivyo ili kukiimarisha chama chetu na Viongozi wake”
Prof. Kitila Mkumbo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji na Mbunge wa Jimbo la Ubungo

Waziri Prof. Kitila amesema Serikali itawashirikisha kikamilifu vijana katika kuandaa Dira ya Maendeleo ya Taifa ambayo itakuwa kwaajili ya miaka zaidi ya 20 ijayo na wahusika wa Dira hiyo ni vijana hivyo hawataachwa katika maandalizi yake ili watoe mawazo yao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Seneti ya Vyuo Vikuu na vya kati mkoa wa Dar es Salaam Yunus Suleiman Hassan amesema wanatumia nguvu zao katika kuleta maendeleo na kuyazungumza yale yanayofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi.

Amesema jukumu lao ni kuongeza wigo wa wanachama vyuoni kwa kufungua matawi mengi zaidi huku wakisema ukweli kwa Viongozi kuhusu utendaji kazi wao kwa lengo la kuwasaidia.

Mwenyekiti wa Tawi la Shule ya Sheria Gurandi Mauta amesema wanao mpango wa kutoa msaada wa sheria kwa wananchi wa Ubungo ili nao baada anufaike na uwepo wa shule hiyo katika eneo lao ikiwa ni sehemu ya kurudisha kwa jamii na tayari wameandaa andiko kwaajili ya zoezi hilo.

Rais wa Shule ya Sheria Gideon naye amehudhuria mkutano huo na kumuomba Mbunge kuwasaidia kutengeneza kipande cha barabara kinachotoka Mawasiliano kwenda chuoni hapo jambo ambalo Prof. Kitila amesema kuwa barabara hiyo ni miongoni mwa barabara ambazo zipo kwenye mradi wa DMDP na itajengwa kwa kiwango cha lami.

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!