Home Kitaifa PROF. KITILA AWAPONGEZA JUKWAA LA WANAWAKE KIMARA KWA UBUNIFU

PROF. KITILA AWAPONGEZA JUKWAA LA WANAWAKE KIMARA KWA UBUNIFU

Na Rahel Chizoza, DSM

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji na Mbunge wa Jimbo la Ubungo Prof. Kitila Mkumbo ameupongeza uongozi wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi Kata ya Kimara kwa ubunifu wa kujenga vyumba vya wasichana kujisitiri kwenye shule Sita za msingi na Sekondari za Serikali zilizopo katika Kata ya Kimara.

Akizindua Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake katika mtaa wa Kilungule Kata ya Kimara Dar es Salaam Prof. Kitila Mkumbo amesema wazo la kujenga vyumba hivyo litawasaidia wasichana kuhudhuria masomo muda wote na hivyo kupunguza changamoto ya utoro kwa Watoto wa kike.

“Mmefanya jambo kubwa ambalo linapaswa kuwa mfano kwa mkoa wa Dar es Salaam na nchi nzima kwa ujumla” amesema Prof. Kitila Mkumbo.

Kutokana na jitihada zilizofanywa na Wanawake hao, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amewachangia kiasi cha Sh. 500,000 na kuahidi kuwachangia zaidi kupitia fedha za mfuko wa Jimbo mpaka pale lengo lao litakapotimia.

Sambamba na uzinduzi wa Jukwaa hilo pia Prof. Kitila Mkumbo ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa vyumba hivyo vya wasichana ambapo kila chumba kitagharimu kiasi cha Sh. Milioni 2.5.

Awali akizungumza katika mkutano huo Diwani wa Kata ya Kimara Mhe. Ismail Mvungi amesema atatoa matofali ya kukamilisha ujenzi wa chumba kilichowekewa jiwe la msingi na kusimamia ujenzi katika vyumba vyote sita ambavyo Yeye ndiyo ametoa mchoro.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!