Home Kitaifa ONGEZEKO IDADI YA MABWENI, LAONGEZA UDAHILI WA WANAFUNZI WA KIKE YAKOBI

ONGEZEKO IDADI YA MABWENI, LAONGEZA UDAHILI WA WANAFUNZI WA KIKE YAKOBI

Na Jacquiline Mrisho – Maelezo

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Bweni ya Yakobi iliyopo katika Kijiji cha Limage, Halmashauri ya Mji Njombe mkoani Njombe, Editor John amesema kuwa kutokana na Serikali kupeleka fedha kwa ajili ya kuongeza mabweni, udahili wa wanafunzi umeongezeka kutoka wanafunzi 105 hadi 433.

Ameyazungumza hayo hivi karibuni wakati akihojiwa na Maafisa Habari kutoka Idara ya Habari (Maelezo) ambapo amesema kuwa, jumla ya shilingi milioni 543 zilipelekwa na Serikali kwa ajili ya upanuzi wa miundombinu ya elimu kwa ajili ya kidato cha tano na sita ambapo fedha hizo zimeweza kujenga mabweni matatu ya watoto wa kike, madarasa matano pamoja na matundu 14 ya vyoo.

“Tulifanikiwa kutekeleza ujenzi wa mabweni matatu ambayo yamekamilika na wanafunzi wanaishi, madarasa matatu, ofisi moja, matundu 16 badala ya 14 pamoja na samani za ndani ya mabweni ambapo ilitakiwa kununua vitanda vya deka 120 lakini kupitia matumizi mazuri ya fedha hizo, vilinunuliwa vitanda vya deka 180 na badala ya kununua viti 200 na meza 200, imewezekana kununua viti 380 na meza 380, alisema  bi. Editor.

Bi. Editor ameongeza kuwa, mnamo mwezi Agosti, 2023 Serikali ilileta tena jumla ya shilingi milioni 130 kwa ajili ya ujenzi wa bweni lingine la wasichana ambalo linakaribia kukamilika. Aidha, ameishukuru Serikali kwa ujio wa fedha hizo kwani sio mara ya kwanza kuwakumbuka, hata kipindi cha kwanza cha kuanzisha kidato cha tano na cha sita, ilipeleka jumla ya shilingi milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa bweni ambalo kwa kiasi kikubwa limewasaidia wanafunzi kusoma katika mazingira bora na wote kufaulu kwa daraja la kwanza hadi la tatu.

Kwa upande wake mwanafunzi, Amokile Sanga amesema kuwa, mabweni hayo yamekuwa msaada mkubwa kwani wanalala vizuri bila kubanana na ni mabweni bora kwa kuwa yamejengwa kisasa, ameeleza kuwa taaluma bora huwa inaendana na miundombinu bora hivyo kuongezeka kwa mabweni hayo kumewasaidia kuwa na taaluma bora.

Uwepo wa mabweni haya umesaidia watoto wa kike kuwa na mazingira bora ya kupata elimu kwani wasichana wengi wanaosoma shule za kutwa hukutana na vikwazo vingi njiani ambavyo hukatisha ndoto zao za kupata elimu,” alisema Amokile.

Naye mwanafunzi Nancy Abraham amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani pamoja na ujenzi wa mabweni uliosababisha udahili wa wanafunzi kuongezeka, bado alitoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu na madarasa matano yanayoendana na wingi wa wanafunzi hao.

Akizungumza kwa ujumla, Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Mji Njombe, Mwalimu Prochesius Mguli amesema kuwa Serikali imeleta fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu ambapo kwa mwaka 2022/23, Halmashauri ya Mji Njombe ilitekeleza baadhi ya miradi ikiwemo ujenzi wa nyumba za Walimu (2 in 1) katika Shule ya Sekondari Lunyanywi ambapo zililetwa jumla ya shilingi milioni 100 na tayari ujenzi wake umeshakamilika, pia kupitia mradi wa SEQUIP, Serikali imeleta shilingi milioni 583.1 ambayo imetumika kujenga shule ambayo itaanza rasmi mwaka 2024.

Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!