Na Shomari Binda-Butiama
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Butiama Baraka Imanyi maarufu “Obama” amesema kuna umuhimu mkubwa kupanda na kutunza miti kwa uhifadhi wa mazingira.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa maadhimisho ya miaka 47 ya CCM yaliyoazimishwa na kimkoa na jumuiya ya wazazi mkoani Mara.
Akizungumza na wanafunzi na walimu wa shule ya sekondari Bumaswa mara baada ya zoezi la upandaji miti amesema suala la uhifadhi wa mazingira lina umuhimu mkubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Amesema miti iliyopandwa na vyema ikatunzwa na kukua sababu itakuwa na manufaa makubwa kwa shule, jamii inayozunguka shule na jamii kwa ujumla.
Obama amesema miti ya matunda, kimvuli na mbao iliyopandwa wanafunzi watakuja kula matunda kwaajili ya afya na kupata pesa mbao zitakapokuja kuuzwa.
“Leo kama jumuiya ya wazazi mkoa wa Mara tunaadhimisha miaka 47 ya CCM moja ya shughuli tuliyofanya ni kupanda miti kwenye shule hii kwaajili ya uhifadhi wa mazingira.
“Naomba wanafunzi pamoja na walimu tuitunze miti hii kwa kuwa itakuja kutusaidia hapo baadae na kutunza mazingira yetu“,amesema Obama.
Mwenyekiti huyo wa jumuiya ya wazazi wilaya ya Butiama amewasisitiza wanafunzi kutojiingiza kwenye vitendo visivyokuwa na maadili.
Amesema jumuiya ya wazazi inalo jukumu la kuhakikisha maadili yanazingatiwa na wataendelea kuyasimamia kwenye jamii.
Aidha Obama amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha wavuvi wa mkoa wa Mara kupata vizimba na boti za kisasa kwa shughuli za uvuvi.