Na Shomari Binda-Musoma
MCHEZO wa kutafuta mshindi wa 3 wa mashindano ya Mathayo Cup utafanyika kesho saa 10 jioni kwenye uwanja wa Mara sekondari.
Timu za Nyakato fc na Makoko fc zitavaana kwenye mchezo huo katika kuwania zawadi za mshindi wa 3.
Nyakato iliondolewa na timu ya Nyamatare kwenye mchezo wa nusu fainali kwa kufungwa kwa mikwaju ya penati 4-2 huku Makoko ikiondolewa na Mwigobero fc kwa penati 3-2 baada ya michezo yote kumalizika dakika 90 bila mshindi
Katibu wa mbunge wa jimbo la Musoma mjini Christopher Majala amesema maandalizi ya mchezo huo yanaendelea vizuri.
Amesema katika mchezo huo utahudhuriwa na mbunge wa jimbo la Musoma mjini Vedsstus Mathayo ambaye atapata fursa ya kuzungumza na wanamichezo uwanjani hapo.
Majala amesema moja ya mambo ambayo mbunge atakayozungumzia ni pamoja na kutangaza mpangilio wa zawadi za washindi wa msimu huu.
Wakizungumzia mchezo huo timu zote zimesema huo ndio mchezo wa kufutia machungu baada ya kushindwa kuingia fainali.
Meneja wa timu ya Nyakato Zakayo Zakayo amesema lengo lilikuwa ubingwa na wameshindwa kufikia na nafasi pekee ni kushinda mshindi wa 3.
Upande wa timu ya Makoko kupitia mmoja wa viongozi wake Mwalimu Kennedy amesema wanakwenda kumaliza hasira zao kwa Nyakato.