Na Shomari Binda
Mwenyekiti wa Chama cha Demikrasia na Maendeleo ” Chadema” Wilaya ya Butiama Michael Makenji ameonyesha msimamo wa kumchagua Tundu Lissu kwenye uchaguzi wa chama hicho unaofanyika leo.
Huu ni uchaguzi wa kihistoria unaofanyika ndani ya chama hicho ambao mvutano umeonekana kati ya Mwenyekiti wa chama hicho wa sasa Freeman Mbowe na Makamu Mwenyekiti Tundu Lissu.
Akizungumza na kituo kimoja cha televisheni kutoka ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salam Makenji amesema ametumwa na wanachama Wilaya ya Butiama kumchagua mgombea huyo.
Amesema wanaimani Lissu ataleta mabadiliko ndani ya chama hicho na kufikia malengo ya chama hicho ikiwa ni pamoja na kushika dola.
Makenji amesema Lissu ataleta tumaini jipya na ndio kilichopelekea kuwa na imani naye kuelekea uchaguzi huo.
Amesema mvutano hupo kwenye uchaguzi kwa pande zote mbili kubwa za wagombea lakini wanayo nafasi kubwa kushinda upande wao.
” Mchakato unaendelea vizuri hapa ukumbini na Butiama tunakwenda na Tundu Lissu kwenye uchaguzi huu unaofanyika leo.
” Kikubwa ni baada ya uchaguzi kuwa wamoja na kwenda kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 tukiwa wamoja”,amesema Makenji.
Baadhi ya wajumbe wanaoshiriki uchaguzi huo wamesema wanakwenda kuwachagua watu sahihi kwa nafasi ya Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti watakao kivusha chama hicho.