Home Kitaifa NHC YAZIDI KUIMARIKA, UJENZI WA MIRADI MBALIMBALI WAENDELEA

NHC YAZIDI KUIMARIKA, UJENZI WA MIRADI MBALIMBALI WAENDELEA

*Mapato yafikia Bilioni 257 kutoka billion 144 mwaka 2021/2022

*Sera ya Ubia Kupaisha Sekta ya Makazi

Na Beatrice Sanga-MAELEZO

Shirika la Nyumba nchini (NHC) limeeleza kuwa litaendelea kutengeneza faida kutokana na kushiriki katika shughuli na miradi mbalimbali ikiwemo ushauri elekezi, ujenzi wa nyumba, uendelezaji wa mipango miji katika mikoa mbalimbali ambapo mpaka sasa mapato ya Shirika hilo yameongeza kutoka bilioni 144.42 kwa mwaka 2021/2022 hadi kufikia bilioni 257.47.

Hayo yamesemwa August 3, 2023 na Hamad Abdallah Hamad Mkurugenzi Mkuu Shirika la Nyumba la Taifa wakati wa Mkutano na Wahariri wa Vyombo vya Habari uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JINCC) Jijini dar es salaam uliolenga kuelezea mafaniko mbalimbali na kuweka bayana mpango kazi wa utekelezaji wa shughuli zake kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Shirika hilo limesema kuwa litaendelea na shughuli za ujenzi, uuzaji na usimamizi wa maendeleo ya nyumba na makazi ili kuhakikisha kila mtanzania anakuwa na makazi bora, salama na imara huku pia likitengeneza faida kutokana na kupangisha, kujenga na kuuza nyumba za makazi na biashara kwa mtu mmoja, taasisi ama kampuni binafsi ambapo mauzo ya nyumba yamepanda na kufikia zaidi ya bilioni 120.

Shirika la Nyumba la Taifa limeendelea kuongeza mapato yake hadi kufikia kiasi cha shilingi bilioni 257.47 kwa mwaka 2022 ikilinganishwa na mwaka 2021 ambapo mapato yake yalikuwa bilioni 144.42, Mwaka 2021/22, mapato ya kodi yamepanda na kufikia shilingi bilioni 90.76 kutoka shilingi bilioni 89.23 mwaka 2020/21, Mauzo ya nyumba yamepanda kutoka Shilingi bilioni 29.33 mwaka 2020/21 na kufikia shilingi bilioni 121.95 mwaka 2021/22, Mapato miradi ya Ukandarasi yamekua kutoka shilingi bilioni 25.60 mwaka 2020/21 hadi kufikia shilingi bilioni 43.98 mwaka 2021/22.” Amesema Hamad.

Hamad amesema kuwa kwa sasa NHC imeongeza kiwango cha gawio serikalini ikilinganishwa na miaka ya nyuma huku akiamini kuwa kutokana na kuimarika kwa shughuli za ujenzi wa miradi mbalimbali ambayo ni miradi ya kimkakati na ya nyumba za makazi na biashara ikiwemo miradi ya ukandarasi, Ujenzi wa nyumba za makazi, Ukamilishaji wa miradi mikubwa iliyokuwa imesimama, Usanifu na usimamizi wa miradi ya ujenzi, Utekelezaji wa sera ya ubia, Uendelezaji wa vitovu vya miji na Ukusanyaji kodi ya nyumba Shirika hilo litaendelea kuwa chanzo kikubwa cha mapato serikalini.

“Ongezeko hili lilienda sambamba na ongezeko la majengo, kuimarika kwa soko la nyumba, Shirika liliweza kulipa kodi mbalimbali inayofikia takriban shilingi bilioni 32.4 kwa mwaka 2021/2022, Aidha, Shirika limelipa gawio Serikalini la shilingi milioni 750 kwa mwaka 2021/2022, gawio hili ni kiwango kinachopaswa kulipwa na Shirika kila mwaka kutokana na maelekezo ya Msajili wa Hazina.” Ameongeza Mkurugenzi huyo.

Aidha Shirika hilo pia limeendelea kuboresha nyumba zake kwa kuzikarabati katika mikoa mbalimbali nchini ambapo limelenga kufikia ukarabati wa majengo 101 yaliyopo katika mikoa 15 yenye ofisi za NHC kwa mwaka 2023/2024.

NHC imeeleza kuwa, kwa sasa lina mkakati wa kuboresha zaidi sekta ya nyumba nchini kwa kuendelea kuishawishi serikali kuwa nyumba ni kipaumbele cha taifa, na kuwaruhusu Diaspora kununua na kuwekeza katika ardhi ya Tanzania, ikiwa ni utekelezaji wa Majukumu ya Shirika hilo kwa kuzingatia Mpango Mkakati wa Shirika wa Miaka 10 (2015/16–2024/25) ambao unalenga kuwezesha ujenzi wa nyumba na kusimamia rasilimali nyumba za Shirika.

Tunaendelea kuishawishi Serikali kuondoa vikwazo vyote vinavyowazuia Watanzania wanaoishi ughaibuni pamoja na raia wa mataifa mengine kushiriki katika kuwekeza kwenye sekta ya uendelezaji miliki.” Amesema Hamad.

Kwa upande mwingine Hamad amesema sera ya ubia kati ya serikali na sekta binafsi yenye malengo ya kuongoza na kusimamia utekelezaji wa miradi kwa ushirikiano kati ya Shirika na Sekta Binafsi katika kuendeleza maendeleo ya makazi na mipango miji nchini kwa ufanisi zaidi, ambapo mpaka sasa kuna miradi inayotarajiwa kutekelezwa ambayo itaongeza idadi ya nyumba za kuishi pamoja na maeneo ya biashara na hivyo kuchangia kutatua changamoto ya Makazi na majengo bora ya biashara.

Shirika limehuisha na kuizindua sera ya ubia ili kushirikisha wadau mbalimbali kuendeleza sekta ya makazi na kuongeza makazi bora kwa ajili ya Watanzania, uzinduzi wa Sera ya Ubia umefungua milango ya uwekezaji kwenye sekta ya nyumba na kuunga mkono maono na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuvutia uwekezaji nchini kupitia sekta binafsi ambayo ni injini ya kujenga uchumi imara.”

Shirika la Nyumba la Taifa lilianzishwa mwaka 1962 kwa sheria ya Bunge Namba 45 kwa malengo ya kuwapatia watanzania makazi bora lakini pia kuzalisha na kuwezesha uzalishaji, kusimamia miliki za majengo yake na wamiliki wengine lakini pia kuendesha shughuli za ujenzi na kutoa ushauri katika masuala ya ujenzi.

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!