Na Mercy Maimu
Shirika la nyumba la Taifa NHC linatarajia kuzindua sera ya Ubia inayoenda kufungua milango ya uwekezaji kwenye sekta ya nyumba kwa kuruhusu sekta binafsi ambayo ni injini ya kuleta na kujenga uchumi wa Taifa letu.
Hayo yamesemwa na Meneja Habari na Uhusiano wa Shirika la nyumba la Taifa NHC MUUNGANO SAGUYA wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam kuhusu matayarisho ya uzinduzi wa sera hiyo na kueleza kuwa mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu KASSIM MAJALIWA. Amesema uzinduzi huo wanatarajia kushirikisha takribani washiriki 1000 kutoka Taasisi mbalimbali za serikali na binafsi, vyama na Bodi za kitaaluma pamoja na wawekezaji binafsi wa ndani na nje ya Nchi.
“Baada ya kuanza kuutangazia Umma juu ya jambo hilo jema la uzinduzi wa Sera hiyo, kumekuwa na muitikio mkubwa wa makampuni binafsi ya ndani na nje ya nchi wa kushiriki uzinduzi huo”amesema Saguya.
Aidha amesema kumekuwa na utayari mkubwa wa makampuni na Taasisi binafsi za nje na ndani ya Nchi kutaka kuwekeza katika ujenzi wa majengo makubwa katika viwanja vya NHC ambapo kutokana na hali hiyo Shirika litachambua na kuainisha zaidi maeneo ya kutosha ya kukidhi shauku hiyo ili kuendelea kujenga Nchi.
“Kumekuwa na utayari mkubwa wa Makampuni na taasisi binafsi za nje na ndani ya nchi kutaka kuwekeza katika ujenzi wa majengo makubwa kwenye viwanja vya NHC. kutokana na hali hiyo, Shirika limeona ni vema kuchambua na kuainisha zaidi maeneo ya kutosha ya kukidhi shauku hiyo ya kujenga nchi yetu. hapo hawali tulitenga maeneo 60 tu yenye viwanja/majengo yanayohitaji kuendelezwa. Kwa msukumo uliopo sasa tumeamua kuongeza maeneo zaidi ili yaendelezwe” amesema Saguya.
Uzinduzi huo utafanyika tarehe 16 November 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere .