Home Kitaifa NGORONGORO YASISITIZA KUENDELEA KUHAMISHA WANANCHI WANAOJIANDIKISHA KUHAMA KWA HIYARI.

NGORONGORO YASISITIZA KUENDELEA KUHAMISHA WANANCHI WANAOJIANDIKISHA KUHAMA KWA HIYARI.

Na Mwandishi wetu, Arusha.

Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) imesema itaendelea kuelimisha, kuthaminisha na kuhamisha wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi ya Ngorongoro ambao wanajiandikisha kuhama kwa hiyari yao wenyewe na haitayumbishwa na kelele za baadhi ya vikundi vya watu wanaowatumia wananchi hao kupata kipato kupitia baadhi ya mashirika duniani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha mwishoni mwa wiki kaimu meneja wa uhusiano kwa umma wa mamlaka hiyo Hamis Dambaya amesema mpaka sasa zoezi linakwenda vizuri na wananchi wengi wanataka kutoka katika eneo hilo ambapo serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa nyumba 5000 katika Vijiji vya Msomera, Saunyi na Kitwai.

Ujenzi wa Nyumba hizo unaenda sambamba na ujenzi wa miundo mbinu mingine ya huduma za kijamii ili kuhakikisha wananchi hao wanapohama wanakuta Serikali imeboresha huduma zote za kijamii katika mazingira salama zaidi tofauti kuishi na wanyama wakali ndani ya hifadhi.

Dambaya amesema kasi ya ujenzi wa nyumba hizo inayofanywa na Jeshi la Kujenga Taifa katika vijiji hivyo inakwenda vizuri na takribani kila siku nyumba zinakamilika huku zoezi la kuelimisha wananchi kuondoka ndani ya hifadhi ya Ngorongoro nalo likiendelea kufanyika ili kuhakikisha kila mwananchi anayetaka kuhama anaondoka bila kuchelewa.

Zoezi letu tunalifanya kwa uangalifu mkubwa kwa kutumia vyombo vya kiserikali ili kuhakikisha kuwa hakuna mtu ambaye anahamia kutoka sehemu nyingine nchini au nchi Jirani anahamishwa hasa ikizingatiwa kuwa wananchi wengi wanaona zoezi hilo ni fursa ya kukuza uchumi na maisha yao kulinganisha na maisha ndani ya hifadhi na inapobainika mwananchi ameghushi makazi na kuhamishwa atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi,”alisema Dambaya.

Kuhusu madai ya baadhi na NGO’s kudai kuna ukiukwaji wa haki za binadamu katika zoezi hilo, Dambaya amesema Serikali iko makini naninafuata sheria, kanuni, taratibu, misingi ya utawala bora, haki za binadamu na kuzingatia malengo la milenia ili kuboresha maisha ya wananchi hao.

Amesema Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro haijawahi kumuondoa mtu kwa nguvu kutoka ndani ya hifadhi na ndio maana hata baadhi ya taasisi zinazotoa madai hayo zimekuwa zikipiga kelele zikiwa nje ya Tanzania na wengi wao hawana upeo kuhusu maisha ya wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi.

Itakumbukwa kwamba wakati hifadhi hiyo inaanzishwa mwaka 1959 ilikuwa na wakazi elfu 8000 tu ambapo mpaka kufikia sasa hifadhi hiyo ina zaidi ya watu laki 110,000 jambo ambalo limewafanya waishi maisha magumu kutokana na kukosa maeneo ya kufanyia shughuli zao za kimaendeleo kwa kuwa wakati idadi ya Wananchi, shughuli za kibinadamu na wanyamapori zikiongezeka eneo la hifadhi limebaki na ukubwa uleule hali inayosababisha migongano ya wananchi na Wanyamapori.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!