Home Kitaifa NGORONGORO WASISITIZWA KUACHA KUTUNZA FEDHA NYUMBANI

NGORONGORO WASISITIZWA KUACHA KUTUNZA FEDHA NYUMBANI

Na. Saidina Msangi, WF, Ngorongoro, Arusha.

Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro wametakiwa kutumia huduma rasmi za fedha kutunza fedha zao badala ya kutunza nyumbani ili ziweze kuingia katika mzunguko wa fedha na kuongezeka thamani.

Rai hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Bw. Hussein Urughu, alipokuwa akifungua mafunzo ya elimu ya fedha, wakati Timu ya Maafisa kutoka Wizara ya Fedha iliyoambatana na Maafisa kutoka taasisi na watoa huduma za Fedha ilipowasili kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha na kuhamasisha utumiaji wa huduma za fedha zilizo rasmi katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro. 

Alisema kuwa njia ya kutunza fedha nyumbani si salama kutokana na kuweza kupata hasara kutokana na majanga ya moto au kuibiwa na hivyo kushauri wananchi kutumia huduma za benki kutunza fedha ili ziingie katika mzunguko watu wapate mikopo ili kukuza uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

‘’Watu wanauza mifugo wanakaa na fedha nyumbani ambapo wangeweza kuweka sehemu nyingine ikazaa faida, wengine wanaingia vikundi vya kukopeshana bila kufuata taratibu na baadaye wanadhulumiwa, hivyo ni matarajio yetu kuwa elimu ya fedha mtakayoitoa itawafungua wananchi kuondokana na changamoto hizo,’’alisema Bw. Urughu.

Alisema kuwa masuala ya fedha yanafanyika kimazoea katika jamii kwani sheria kanuni na taratibu za fedha hazifuatwi hivyo elimu ya fedha ni chachu kwa wananchi wa Ngorongoro kupata uelewa wa namna bora ya kutunza na kutumia fedha zao kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu.

Aidha, alisema kuwa elimu ya fedha itawasaidia wananchi kuweza kujua namna ya kuweka akiba, umuhimu wa bima, jinsi ya kuwekeza pamoja na kujipanga vema kutumia fursa za mikopo inayotolea na Halmashauri ili kuweza kujikwamua kiuchumi.

Naye Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, alieleza kuwa ni muhimu kila mwananchi kuhakikisha kuwa wanachukua mkopo katika taasisi za fedha zilizosajiliwa na Benki Kuu ya Tanzania.

‘’Unapoenda kukopa hakikisha kuwa taasisi imesajiliwa na Benki Kuu ya Tanzania lakini pia ni muhimu kuangalia riba ili kujiepusha na riba zisizofuata sheria kanuni na taratibu ambazo ndio zinasababisha kuwa na mikopo inayojulikana kama kausha damu kwani riba ni kandamizi,’’, alisisitiza Bw. Kibakaya.

Aidha, Bw. Kibakaya aliwaeleza wananchi hao kuwa bila kujali aina ya shughuli wanazofanya uwekaji wa akiba ni muhimu kwa maisha ya sasa na baadaye hivyo ni vema kuwa na mipango ya mapato na matumizi huku wakitoa kipaumbele katika upande wa kuweka akiba.

Naye Afisa Sheria Mwandamizi kutoka Kurugenzi ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Ramadhani Myonga, alisisitiza kuwa dhamana zinazowekwa kwa ajili ya mikopo ni lazima zifanyiwe tathmini ili kujua thamani halisi ya mali inayowekwa dhamana.

‘’Unapotaka kuweka dhamana kwenye mali ambazo hazihamishiki usiweke hati ya kiwanja au nyumba bila kutathmini kujua thamani halisi kwani endapo utashindwa kurejesha mkopo maafisa wasio waaminifu wanaweza kusababisha mali hiyo kuuzwa kwa bei rahisi ukafilisika na mkopo unakuwa haujaisha,’’ alisisitiza Bw. Myonga.

Timu ya Maafisa kutoka Wizara ya Fedha iliyoambatana na Maafisa kutoka taasisi na watoa huduma za Fedha inaendelea na programu ya elimu ya fedha kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro ambapo makundi ya wakulima, wafungaji, na wajasiriamali yanatarajiwa kufikishiwa elimu hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!