Mbunge wa Jimbo la Kigamboni Mhe. Dkt Faustine Ndugulile akizungumza na wana Kigamboni katika Tamasha la KigamboniPatamu, ameonesha matamanio yake ya kuifanya Kigamboni kuwa Dubai au Guangzhou ya Tanzania.
Dkt Ndugulile alisema kuwa Kigamboni ina ardhi ya kutosha, ukanda wa bahari wenye urefu wa 70km na bandari iliyo karibu na Wilaya hiyo. Hivyo, aliitaka Serikali kufikiria kuiwezesha Kigamboni kuwa kitovu cha utalii na uwekezaji nchini.
Aidha, alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa miradi mingi ambayo anaielekeza Kigamboni na kuifanya kuwa Wilaya inayokua kwa kasi zaidi nchini.
Mgeni Rasmi katika hafla hii, Waziri wa Fedha Mhe Mwigulu Nchemba alisema kuwa amepokea wazo na kwamba wataenda kulichakata ndani ya Serikali.
Tamasha la Kigambonipatamu limeandaliwa na Serikali ya wilaya chini ya Mkuu wa Wilaya Mhe Halima Bulembo kwa lengo la kukuza uwekezaji ndani ya Kigamboni.