Home Biashara NCHI ZA AFCFTA ZASHAURIWA KUBORESHA MIUNDOMBINU, MAZINGIRA YA BIASHARA NA USHIRIKIANO WA...

NCHI ZA AFCFTA ZASHAURIWA KUBORESHA MIUNDOMBINU, MAZINGIRA YA BIASHARA NA USHIRIKIANO WA KIKANDA.

Na Suzan Mshakangoto na Joseph Nelson

Makamu wa Pili wa Rais, wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amezishauri Nchi wanachama wa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA) kuhakikisha kuwa miundombinu ya barabara, reli, bandari, na viwanja vya ndege inaboreshwa ili kuwezesha biashara na usafirishaji wa bidhaa na huduma kwa urahisi.

Ameyasema hayo Juni 25, 2024 wakati akifungua Mkutano watatu (3) Maalumu wa Mawaziri Mkutano wa 14 wa Baraza la Mawaziri wa AfCFTA uliofanyika Juni 24 – 25, 2024, Zanzibar, ambapo Tanzania ni Mwenyekiti wa Mikutano ya ngazi zote kwa mwaka 2024 na iko tayari kushirikiana na Nchi zote wanachama wa AfCFTA ili kuhakikisha kuwa biashara na uwekezaji Barani Afrika vinaimarika na kuleta maendeleo kwa ujumla.

Aidha, ametoa wito kwa nchi hizo pia Kuwezesha Biashara Ndogo na za Kati (SMEs) ambazo zinabeba zaidi ya asilimia 70% ya Uchumi kwa kuziwekea mazingira rafiki kwa biashara, kurahisisha upatikanaji wa mikopo nafuu, elimu ya biashara na masoko ili ziweze kushiriki kikamilifu katika biashara za kikanda na kimataifa.

Makamu wa Pili wa Rais pia amezishauri Nchi hizo pia kuimarisha ushirikiano wa kikanda na baina ya nchi ili kuwa na sera za uchumi na biashara zinazoendana na kusaidiana, Kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kupunguza urasimu, kuimarisha utawala bora, na kuhakikisha usalama wa mitaji na mali za wawekezaji.

Vile vile amezitaka Nchi hizo kujenga uwezo wa watu kwa kuwekeza katika elimu, afya, na mafunzo ya kiufundi ili kuhakikisha kuwa kunakuwa na nguvu kazi yenye ujuzi na uwezo wa kushindana katika soko la kimataifa, kukuza biashara ya ndani ya Afrika na kusaidia katika kuboresha maisha ya wananchi, na kuongeza mapato ya taifa.

Makamu wa Rais pia amezishauri Nchi hizo kuzingatia masuala ya kijamii na kimazingira ili kuhakikisha kuwa ukuaji wa kiuchumi unakwenda sambamba na maendeleo endelevu na kujali Mazingira na kuhakikisha kuwa faida za AfCFTA zinawafikia watu wote, na si kundi dogo tu la watu.

Aidha, Makamu wa Rais pia amewashauri mawaziri hao wa Biashara AfCFTA kuhakikisha majadiliano na maamuzi yanalenga kuunganisha Bara la Afrika, kukuza biashara za ndani na za kimataifa ili kutimiza malengo ya Agenda 2063 ya Afrika tunayoitaka na ndoto za Waasisi wa Bara la Afrika akiwemo Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, ambao walikuwa na ndoto ya kuona Nchi za Afrika zinaungana na zinajitegemea kiuchumi

Akiwahamasisha Watanzania kuchangamkia fursa za AfCTA, amebainisha kuwa Tanzania ina Kampuni zaidi ya Kumi na Moja (11) zinazofanya biashara Afrika kwa kutumia Cheti cha Uasili wa Bidhaa cha AfCFTA kwa kusafirisha Nyuzi za Katani kwenda nchini Nigeria, Misri, Ghana na Morocco; Kahawa kwenda nchini Algeria; na Tumbaku kwenda nchini Nigeria ambapo baadhi ya Kampuni hizo zinaongozwa na Wanawake.

Aidha, amemtaja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Kinara (Champion) wa Wanawake na Vijana Afrika kuwa amekuwa akitoa msisitizo wa mara kwa mara kwa Jamii ya Wafanyabiashara kuchangamkia fursa za Kikanda ikiwemo AfCFTA ikiwemo kuongeza bajeti kwenye Sekta za Uzalishaji ili kuhakikisha ushiriki wa Tanzania kwenye biashara ndani ya Afrika utaendelea kukua na kuimarika zaidi.

Naye Katibu Mkuu wa AfCFTA Mhe. Wamkele Mene amebainisha kupitishwa kwa Itifaki za Biashara ya Kidigitali na Wanawake na Vijana katika Biashara katika Kikao cha 37 cha Wakuu wa Nchi za AU kumefungua njia ya ushirikiano wa kiuchumi wa Bara la Afrika na kumekuwa na ongezeko la Nchi zinazoonyesha nia ya kujiunga na AfCFTA.

Aidha, alibainisha kuwa Sekretarieti ya AfCFTA imeanza kukusanya takwimu za kila mwezi na za mwaka kuhusu biashara chini ya utawala wa AfCFTA ili kufuatilia utendaji na kuelewa mwelekeo wa biashara na mapitio ya kwanza ya AfCFTA yanayotarajiwa mwaka huu yataendana na maadhimisho ya miaka mitano ya utekelezaji wake, ambapo tathmini ya kina itafanyika kuhusu athari za mkataba na kutoa mwongozo kwa maboresho ya baadaye.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar Mhe. Shariff Ali Shariff, akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kufungua Mkutano huo amewakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kuwekeza Tanzania na amewahimiza Waafrika kusimamia utekelezaji wa AfCFTA kwa kutumia rasilimali za Afrika kwa maendeleo endelevu na kusisitiza kuwa AfCFTA ni fursa pekee ya kuimarisha biashara na uzalishaji na ushirikiano wa kiuchumi barani Afrika ni muhimu.

Naye Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Mhe. Omar Said Shaaban amesisitiza kuwa kuwa AfCFTA ni msingi wa maendeleo ya kiuchumi, kisiasa, na kitamaduni barani Afrika na kutoa wito kwa Nchi wananchama wote kuhakikisha wanatekeleza makubaliano ya Mkataba huo kwa vitendo.

Aidha, ameeleza kuwa utekelezaji wa AfCFTA umeanza kuzaa matunda, ambapo biashara kati ya nchi za Afrika kwa kutumia taratibuna vigezo vya AfCFTA imeanza kuongezeka japokuwa kuna changamoto kama miundombinu duni, uzalishaji hafifu, nishati, na gharama za mawasiliano ambazo zinapaswa kutatuliwa ili kufikia malengo ya Afrika tunayoitaka .

Akitoa mfano wa miradi inayotekelezwa Tanzania kama hatua za kupunguza changamoto hizo, alifafanua kuwa Tanzania inaendelea na ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR ambayo itaunganisha biashara na usafirishaji na nchi jirani na ujenzi wa Kituo Kikubwa cha kuzalisha umeme cha Mwalimu Nyerere ili kuwa na nishati ya uhakika kwenye uzalishaji na shughuli za biashara na hatimaye kukuza biashara na nchi jirani na Bara la Afrika kwa ujumla

Aidha, akibainisha baadhi ya maeneo yaliyojadiliwa katika Mkutano Maalum wa tatu (3) wa Mawaziri wa Biashara wa AfCFTA uliofanyika siku iliyotangulia, alibainisha kuwa Mawaziri hao walijadili masuala muhimu kama mabadiliko ya hali ya hewa na mapinduzi ya kijani ya maendeleo ya viwanda Afrika na uzalishaji wa vipuri vya magari barani Afrika inayokuwa kwa kasi itakavyonufaisha Bara la Afrika pamoja na kuchukulia changamoto kama fursa na kuweka mikakati thabiti ya maendeleo endelevu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!