Na Shomari Binda-Musoma
BARAZA la madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma wamemchagua diwani wa viti maalumu Naima Minga kuwa Naibu Meya manispaa ya Musoma.
Naima amechaguliwa kwa nafasi hiyo katika kipindi kingine cha mwaka 2023 na 2024 baada ya kushika nafasi hiyo kipindi kilichopita cha mwaka 2021/2022.
Akizungumza mara baada ya kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo Naima amewashukuru madiwani kwa kuendelea kumuamini na kumchagua tena kwenye nafasi hiyo.
Amesema madiwani wapo wengi lakini kumuamini kwake kumethibitisha namna alivyoshirikiana nao vizuri kipindi kilichopita.
Naima amesema kama alivyokuwa akimsaidia Meya na madiwani katika kipindi kilichopita ataendelea kufanya hivyo katika kipindi kingine.
Amesema kazi ya kuongoza inahitaji ushirikiano na kuwaomba madiwani na wataalamu kuendelea kumpa ushirikiano.
“Nawashukuru sana wahwshimiwa kwa kuendelea kuniamini na kunichagua tena kwenye nafasi ya Naibu Meya”
“Nawaahidi kuendelea kuwapa ushirikiano kama ambavyo nimekuwa nikifanya hivyo katika kipindi kilichopita” amesema Naima.
Aidha Naibu Meya huyo amewaomba madiwani na wataalamu kuendelea kushirikiana katika kufanya kazi za halmashauri zikiwemo za ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Katika uchaguzi huo Naima Minga wa CCM ameshinda kwa kupata kura 18 dhidi ya kura 2 za Goldon Marcus wa Chadema.
Wakati huo huo Meya wa manispaa ya Musoma ameteua wajumbe wa kamati mbalimbali na kudai hajafanya mabadiliko makubwa kwa kuwa zinaendelea kufanya kazi nzuri.