Home Kitaifa Naibu Waziri Kundo Ampongeza Rais Samia Uboreshaji Mazingira ya Tasnia ya Habari

Naibu Waziri Kundo Ampongeza Rais Samia Uboreshaji Mazingira ya Tasnia ya Habari

Na Innocent Natai, WazoHuru Media-Dodoma

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha mazingira mazuri ya tasnia ya Habari nchini.

Amebainisha kuwa katika kipindi kifupi tangu aingie madarakani tasnia ya habari imeimarika, waandishi wa Habari wamekuwa na uhuru wa kutoa Habari na kupata Habari kwa urahisi.

Akizungumza tatehe 17 Februari, 2023 wakati akifungua tamasha la usiku wa Habari Dodoma lililoandaliwa na Chama cha Waandishi wa habari Mkoa wa Dodoma (CPC) na kuhudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe.Rosemary Senyamule,Viongozi wa Vyama vya Siasa, waandishi wa Habari wa mkoa huo na wadau mbalimbali wa sekta hiyo, Mhandisi Kundo amesema kuwa kipaumbele kikubwa cha mwanahabari ni kupata habari hivyo kukosa fursa hiyo hatoweza kufanya kazi yake.

Amesema kuwa Mhe Rais ameonyesha nia ya dhati ya kuisaidia tasnia ya habari kwa kufanya mambo makubwa ikiwemo kuandaa mchakato wa kuendelea kuangalia marekebisho ya sheria ya habari ambapo anaamini pindi utakapokamilika wanahabari watakwenda kufanya kazi zao kwa uhuru bila kuwa na changamoto yeyote.

“Haya mazingira mazuri ya tasnia ya Habari Mheshimiwa Rais ameyaweka vizuri katika misingi ya kisheria ili muweze kuhakikisha mnahabarisha Watanzania kuhusu utekelezaji wa mambo yote yanayofanywa na serikali ya awamu ya sita” almmesema Mhe. Mhandisi Kundo

Ameongeza kuwa wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeweka mikakati ya kutazama uchumi wa wanahabari na vyombo vya habari ili kuona kwa namna gani taifa linaweza kutembea kwa pamoja kiuchumi.

Aidha amewapongeza waandishi wa habari wa Mkoa wa Dodoma kwa kutangaza vyema Mkoa wa Dodoma na shughuli za bunge hivyo kuwafikishia vyema taarifa wananchi na wapiga kura majimboni kwao.

Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe.Rosemary Senyamule amesema kuwa Mheshimiwa Rais amewakumbusha viongozi wa serikali kuwa Haki ya kutoa habari kwa wanahabari ni haki ya msingi na ameelekeza kutolewa kwa habari zinazohitajika na Waandishi kwa manufaa ya nchi.

Aidha ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Waandishi wa Habari kwa kuwapa habari ili kuwarahisishia mazingira ya kazi kwani mkoa wa Dodoma unatambua mchango mkubwa kutoka kwa waandishi kwani wamekuwa chachu ya kutangaza shughuli zinazofanywa kila siku na serikali kupitia Mkoa huo.

Akitoa Shukrani kwa niaba ya Waandishi Ndugu Mathias Canal ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa WazoHuru Media amesema kuwa ni jambo zuri na upekee alilolifanya Mheshimiwa Rais kwa wanatasnia wa habari kwani sasa kuanzisha kwa vyombo vya habari nchini imekuwa si jambo la kawaida tena bali imekuwa ni fursa nyingine ya vijana kujiajiri.

Aidha amewapongeza waandishi wa Habari hao kwa kuanzisha kikundi cha kujikwamua kiuchumi kwa kuwekeza fedha kupitia KIKOBA ambacho punde kitakapoimarika wataanzisha Chama cha Akiba na mikopo (SACCOS)

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!