Na: Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amewaasa vijana nchini kutambua na kuthamini vipaji vyao ili waweze kufikia malengo waliojiwekea na kuleta tija kwenye jamii inayowazunguka.
Naibu Waziri Katambi amesema Julai 23, 2022 wakati wa hafla ya uzinduzi wa Taasisi ya Mzalendo Project Foundation iliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Jijini Dar es Salaam.
Alieleza kuwa, azma ya Serikali ni kuendelea kuwajengea vijana mazingira wezeshi yatakayo wapatia fursa mbalimbali zitakazo wawezesha kujiajiri na kujikwamua kiuchumi.
“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ipo tayari wakati wote kutoa msaada wa hali na mali utakao hakikisha vijana wanapata fursa za ajira na upatikanaji wa mitaji itakayo wawezesha kujishughulisha na kazi ambazo zitaweza kuwaingizia kipato,” alisema Katambi
Aidha, Naibu Waziri Katambi alielezea mikakati ya Serikali katika kusaidia vijana ikiwa ni pamoja na tafiti zilizofanyika kwa lengo la kuangalia namna nzuri ya kupunguza changamoto ya ajira. Pia amefafanua hatua zilizochukuliwa katika kuboresha Sera ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007.
Vile vile, ameelezea hatua zilizochukuliwa na serikali kuhusu mabadiliko ya mitaala ili iendane na uzalishaji wa fursa nyingi za ajira na kuuwasaidia vijana kujiajiri zaidi sambamba na kupata ujuzi na maarifa ya kukabiliana na changamoto za ajira.
Aidha, Naibu Waziri Katambi amepongeza vijana nchini kwa namna wanavyojitoa na kujenga uthubutu wa kufanikisha malengo yao, hivyo amewataka vijana kutambua na kuthamini vipaji vyao ili waweze kutimiza ndoto na malengo yao kwa ustawi wa Taifa lao.
Akizungumza awali, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mzalendo Project Foundation (MZPF), Bw. Enock Mwesiga alisema kuwa lengo la taasisi hiyo ni kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana wa Vyuo vikuu nchini mara baada ya kumaliza elimu yao ya juu, Pamoja na kusaidia vijana kupata ufadhili wa kifedha kutoka taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi ili waweze kutimiza malengo ya mawazo yao ya kijasiriamali na kusaidia jamii na taifa kwa ujumla.
“Taasisi hii ya Mzalendo Project Foundation imekusudia kutoa mafunzo ya kijasiriamali kwa vijana hususan wa elimu ya juu nchini ili waweze kuepukana na suala la utegemezi wa ajira za Serikali badala yake waweze kujiajiri na kuajiri wenzao,” alieleza
Naye, Msanii wa Kizazi Kipya Kala Jeremiah, ameeleza kuguswa na vijana hao ambao wameonyesha uthubutu kwa kuanzisha taasisi hiyo. Hali kadhalika msanii huyo alitoa wito kwa vijana kuthamini muda ili waweze kuambatanisha vyema ndoto zao na malengo.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi ameshiriki katika Kongamano la Sensa na Uchumi lililoandaliwa na MAYODA Economic Development Group ambalo limelenga kuongeza mwamko kwa kutengeneza mabalozi wengi ili kuongeza chachu kwa wananchi kujitokeza kuhesabiwa.
Akiwa katika kongamano hilo, Naibu Waziri Katambi amehamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi Agosti 23, 2022.
MWISHO