Na Hamida Ramadhan, Mzawa Online ApDodoma
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimewataka wanachama wake kuachana na taharuki zinazozagaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mchakato wa kumpata mrithi wa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, Abdulahman Kinana.
Uongozi wa chama umebainisha kuwa nafasi hiyo haigombewi bali inajazwa kupitia mapendekezo rasmi yanayofuata Katiba na taratibu za chama.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, CPA Amosi Makala, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, alisema nafasi hiyo haigombewi wala haijazwi kwa fomu.
Amefafanua kuwa mchakato wa kumpata mrithi unategemea mapendekezo yatakayowasilishwa kwenye kikao cha Kamati Kuu na baadaye Halmashauri Kuu ya Taifa.
Amesisitiza kuwa wanachama waache kueneza taharuki na uvumi kuhusu mrithi wa Kinana kwani muda wa kupendekeza jina rasmi bado haujafika.
“Tayari maandalizi ya kikao hicho yanaendelea chini ya usimamizi wa Katibu Mkuu wa CCM, Emmanuel Nchimbi, ” Amesema CPA Makala
CPA Makala ameongeza kuwa CCM inaendeshwa kwa mujibu wa Katiba na taratibu zake, na nafasi hiyo itajazwa kwa wakati muafaka kupitia utaratibu uliowekwa.
Aidha, alitangaza kuwa Mkutano Mkuu wa CCM unatarajiwa kufanyika Januari 18 hadi 19, 2025, jijini Dodoma. Kabla ya Mkutano Mkuu, kikao cha Kamati Kuu kitafanyika Januari 16, 2025, ambacho kitatoa mapendekezo rasmi.
“Mkutano huo wa CCM utaambatana na vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa, ambapo ajenda zitahusu kufanya uchaguzi wa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, kupokea taarifa ya utekelezaji wa kazi za chama kwa kipindi cha mwaka 2022 hadi 2025, pamoja na taarifa ya utekelezaji wa Ilani kwa pande zote mbili, Bara na Zanzibar, ” Amesema.
Katibu huyo amebainisga kuwa maandalizi yanaendelea vizuri na wanachama wanapaswa kuendelea kuwa na utulivu huku wakiheshimu taratibu na maamuzi ya chama.