Na Mwandishi Wetu.
Taasisi isiyo ya kiserikali My Legacy imekutana na kufanya mazungumzo na wadau kutoka makundi mbalimbali kwaaajili ya kuangalia haki za wanawake, vijana na watu wenye Ulemavu katika upatikanaji wa ardhi lengo ikiwa ni kuweza kushirikiana na wadau wengine kwenye kuangalia haki za makundi hayo kama sehemu ya kutekeleza mradi wao wa kuboresha maeneo ya makazi pamoja na kujifunzia.
Akizungumza wakati wa kikao hicho ambacho kilianza Jana Desemba 18 na kutarajiwa kumaliza Desemba 20 mwaka huu, Mkurugenzi Mtendaji wa My Legacy , Fortunata Temu alisema katika mkutano huo walifanya mapitio ya tafiti mbalimbali ambazo zimefanyika kuweza kubaini changamoto ambazo vijana, wanawake na watu wenye Ulemavu wanazipata katika kutafuta haki ya kumiliki ardhi na Mali nyingine.
“Tunawashirikisha wadau kuhusu mapitio hayo na tunampango wa kufanya uchechemuzi ili kuweza kuboresha changamoto ambazo zimeonekana”
Alizitaja changamoto kadhaa ambazo wamezibaini ambapo alisema Moja ya changamoto hizo ni upatikanaji wa ardhi ambapo mara nyingi kinachotumika kuamua ni Sheria za mila na hasa katika masuala ya urithi wa ardhi kama Mali ambapo mila nyingi na desturi zinawabagua wanawake na zinaona vijana kama bado ni watoto ambao wanatakiwa wakae wasubiri kuja kurithi kwa watoto wao.
Pia alisema Watu wenye Ulemavu kutokana na Hali zao, mtizamo na fikra za jamii wanaonekana kama wategemezi ambapo hawapewi kipaumbele katika.kupewa haki za ardhi hii inatokana na mitizamo potofu au fikra ambazo hazisaidii katika kuwawezesha makundi hayo Ili waweze kujiona Wana haki sawa ya kumiliki ardhi n.k
Kwa upande changamoto za wanawake, Temu alisema ” Wanawake katika upande wa mirathi pamoja na mchango wao mkubwa hakuna kipaumbele kikubwa watapewa”
Kwa upande wake mwakilishi kutoka Tasisi ya Mawakili Vijana Rojas Fungo alipongeza jitihada za My Legacy na hatua waliyochukua kushirikisha wadau mbalimbali ili wawe sehemu ya mchakato wa kuhakikisha kwamba wanafanya uchechemuzi ya kuhakikisha makundi hayo tajwa yanapata haki yao ya msingi ya kumiliki ardhi.
“Ardhi ni suala muhimu sana kwenye maisha ya Binadamu, kwasababuanapata Ardhi, shughuli za kiuchumi, kilimo n.k hivyo ni nyenzo muhimu katika maisha ya Binadamu hivyo tuna Kila sababu ya kwenda kama kumiliki ardhi ni sehemu ya haki ya Binadamu”
“Tunatamani kuona wanawake, vijana na wenzetu wanaoshi na Ulemavu wanapata haki hii ya msingi ya kumiliki kwenye maeneo yao aidha kwa kurithi, kununua, au kugawiwa na serikali”
Naye mwakilishi wa watu wenye Ulemavu, Yahaya Bilali aliiomba serikali iweze kuwapatia Mabalozi wachini ili waweze kupata haki zao zote za msingi kwa wakati ambazo zimekua zinasahaulika kwani wamekua na changamoto nyingi ikiwemo umiliki wa ardhi na vitu vingine ambavyo serikali wamekua wakitoa kwaajili ya watu wenye ulemavu.
Aidha aliiomba serikali kuwakumbuka katika mikopo ambayo wamekua wakiitoa ya asilimia 2 kwa walemavu kuhakikisha wanaipata kwa wakati kwa kuwawekea wawakilishi ambao watakua wanafatilia kwa wakati.