Home Kitaifa MWEMBE LOGISTICS YAENDELEA KUWEKEZA KWENYE UTALII, WAZIRI PINDI AWAPONGEZA

MWEMBE LOGISTICS YAENDELEA KUWEKEZA KWENYE UTALII, WAZIRI PINDI AWAPONGEZA

Na Dickson Mzava

Kampuni ya Mwembe Logistics, inayotoa huduma za usafirishaji wa mizigo na uwakala wa forodha, imeendelea kujizatiti na kuonyesha ubunifu mkubwa katika huduma zake, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukuza sekta ya utalii nchini.

Akizungumza katika Tamasha la Utalii linalofanyika wilayani Same, lililopewa jina la Same Tourism Festival – Season Two, Meneja Mkuu wa Mwembe Logistics, James Tindi, alisema kuwa kampuni yao imejikita zaidi katika kutoa huduma bora za usafirishaji, huku wakipanua wigo wao katika utalii kwa lengo la kuwafikia wateja wengi zaidi.

“Katika hatua hii, tumedhamiria kuwekeza katika sekta ya utalii kwa kuboresha na kupanua huduma zetu. Tumeongeza ubunifu katika usafirishaji wa mizigo na kuanzisha huduma mpya za kusafirisha bidhaa zinazohusiana na utalii, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais katika kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania,” alisema James.

James aliongeza kuwa kampuni hiyo imeshiriki katika matamasha mawili ya utalii, ambayo ni sehemu ya mchango wao katika kukuza sekta ya utalii, huku wakiwahimiza wadau wa sekta hiyo kuongeza ubunifu na ushirikiano katika kukuza uchumi wa nchi.

Kwa upande mwingine, Waziri wa Mali Asili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana, aliipongeza kampuni ya Mwembe Logistics kwa juhudi zao katika kuwa wabunifu na kutoa huduma bora, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza ubunifu katika sekta hiyo, ikiwa ni njia ya kuongeza manufaa kwa taifa.

“Tunaishukuru Mwembe Logistics kwa kujitolea kuwekeza katika utalii. Tunawahimiza wendelee kuongeza ubunifu wao na kupeleka huduma hizi nje ya nchi, kwani ni sehemu muhimu ya kukuza uchumi wa taifa na kukuza sekta ya utalii,” alisema Waziri Pindi.

Tamasha la Same Utalii Festival linatarajiwa kutoa fursa nyingi za kukuza utalii wa ndani na kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi.

Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!