Na Boniface Gideon, MUHEZA
Shirika la Mwambao Coastal Community Network kwa kushirikiana na Halmshauri ya Wilaya ya Muheza mkoani Tanga wamezindua rasmi kampeni inayoitwa ‘MKUBA’ ikiwa ni Mkakati wa Kutunza Bahari. Kampeni hiyo inalenga kuhamasisha na kuiwezesha Jamii Kutunza Bahari kwa kupunguza shughuli za kibinadamu na kulinda rasilimali za viumbe hai vinavyoizunguka Bahari huku Wakazi wa maeneo husika wakiwezeshwa kiuchumi.
Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika mwishoni mwa wiki na kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Muheza, Stella Kategiro,Katika fukwe za Bahari ya Kijiji cha Kigombe,iliyoenda sambamba na kukabidhi fedha Sh.10.5Mil.kwa vikundi 5 vya Wajasiriamali. Fedha hizo zimetolewa na Shirika la Mwambao Coastal Community Network Tanzania.
Stella aliwataka Wakazi wanaoishi Mwambao wa Bahari kuacha tabia ya kufanya uharibifu wa rasilimali za viumbe hai Bahari ili kuongeza uzarishaji wa Samaki.
“mnakata mikoko pia mnavua Samaki kwa uvuvi haramu acheni hizo tabia, tunataka tuongeze kiwango cha uzalishaji wa Samaki mana wanazidi kuadimika, lakini pia tunatakiwa tupande mikoko na Kutunza fukwe kwakuacha kutupa taka ngumu ambazo ni sumu kwa viumbe hai wa majini zikiwemo chupa na mifuko ya plastiki” Alisisitiza Stella
Aidha katika hatua nyingine Stella, aliwataka wanufaika wa Fedha zilitolewa na wahisani kuzitumia kwa malengo yaliyokusudiwa,
“hizi fedha zilitolewa na wenzetu wa Mwambao Coastal Community Network Tanzania, naomba tuzitumie kwa malengo yaliyokusudiwa, msije mkaenda kugawana kununua vijora,tunahitaji fedha hizi zizalishe na ziongeze kipato cha kila mmoja wetu hapa” Aliongeza Stella
Kwaupande wake,Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mwambao Coastal Community Network Tanzania, Said Khalid alisema Shirika hilo linajihusisha na utoaji wa Elimu ya utunzaji rasilimali Bahari na uwezeshaji kwa Jamii inayoishi ukanda wa Bahari Bara na Visiwani.
“Fedha hizi tunazozitoa ni sehemu ya mpango kazi wetu wa kuinua kiuchumi Wakazi wanaoishi Mwambao wa Bahari ili wapunguze shughuli Baharini tunatoa Elimu ya utunzaji rasilimali za viumbe hai Bahari, kuwawezesha kielimu, Nyenzo na fedha kwa Jamii inayozunguka Bahari ili waongeze uzarishaji wa Samaki” alisema Khalid
Alisema kwa Mkoa wa Tanga,mpaka hivi sasa, Vijiji 20 kwenye kata 17 na vikundi 103 vyenye Wanachama 3027 kati yao Wanawake 2119 na Wanaume 908 wamenufaika na Mradi huo wa ‘MKUBA’,
“mpaka sasa mwitikio ni mkubwa sana kwa Jamii, tunaendelea na kawapatia Elimu na kuwawezesha Kiuchumi,kuna hitajika juhudi kubwa na zaziada ili kunusuru rasilimali Bahari, shughuli za kibinadamu zinazidi kuongezeka Baharini na kila mmoja wetu awe mlinzi wa mwenzake ili tunusuru kizazi cha sasa na baadae” Alisisitiza Khalid