Home Kitaifa MUWASA YAPIGA MARUFUKU WANANCHI KUUZA NA KUGAWA MAJI KWA MAJIRANI

MUWASA YAPIGA MARUFUKU WANANCHI KUUZA NA KUGAWA MAJI KWA MAJIRANI

-WANAOTAKA BIASHARA KUBADILISHIWA MATUMIZI

Na Shomari Binda-Musoma

MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) imepiga marufuku wananchi kuuza na kugawa maji kwa majirani.

Licha ya marufuku hiyo kwa wale wanaotaka kufanya biashara wanapaswa kubadilishiwa matumizi kutoka ya kawaida kuwa ya biashara.

Akizungumza kwenye mahojiano maalum na Mzawa Blog ofisini kwake mkurugenzi wa MUWASA mhandisi Nicas Mugisha amesema mamlaka hiyo ndiyo yenye wajibu wa kusambaza na kuuza maji.

Amesema kumeibuka mtindo na mazoea ya wananchi waliounganishiwa maji kuuza na kugawa maji jambo ambalo ni kosa kisheria.

Nicas amesema wananchi wajiepushe kuingia kwenye makosa ambayo yatapelekea kuchukuliwa hatua ambayo adhabu yake ni faini au kifungo jela.

Amesema kama mwananchi ana changamoto ya kisitishiwa huduma ya maji anapaswa kufika ofisi ya MUWASA na kuelezea na kupata ufumbuzi nà kama anataka kufanya biashara ni lazima abadilishiwe matumizi

Mkurugenzi huyo amesema mamlaka ipo tayari kumuunganishia huduma ya maji kila mwananchi nyumbani kwake na akayalipia kadri anavyoyatumia.

“Kuuza au kugawa maji kwa majirani ni kosa kisheria na wananchi hawapaswi kufanya hivyo ili kujiepusha kuingia kwenye makosa”

“Kama kuna mwananchi amesitishiwa huduma anapaswa kuja ofisini tusikie changamoto yake na kuweza kumrejeshea huduma ya maji” amesema.

Aidha mkurugenzi huyo amesema mamlaka baada ya kupata mabomba inaendelea na zoezi la usambazaji wa huduma ya maji kwenye mitaa ya pembezoni ya manispaa ya Musoma.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!