Na Shomari Binda-Musoma
MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini Profesa Sospeter Muhongo ameongoza harambee ya mafanikio ya ujenzi wa shule ya sekondari kisiwa cha Rukuba.
Mafanikio ya harambee hiyo ni kujitoa kwa wadau mbalimbali wakiwemo wananchi wa kisiwa hicho kuchangia mifuko ya saruji.
Kwenye harambee hiyo jumla ya mifuko 484 ilipatikana pamoja na fedha taslim shilingi 248,000.
Katika mifuko hiyo ya saruji mbunge Profesa Sospeter Muhongo amechangia mifuko 200,wananchi wazaliwa kisiwa cha Rukuba mifuko 167,kamati ya siasa Kata mifuko 22,kamati ya siasa wilaya mifuko 15,Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya na wenzake mifuko 22 na mkuu wa wilaya na wenzake mifuko 62.
Kisiwa cha Rukuba ni moja ya vijiji vinne (4) vya Kata ya Etaro ambapo wanafunzi wa sekondari kutoka kisiwani humo wanasoma nchi kavu kwenye sekondari ya Kata yao ya Etaro sekondari.
Wanafunzi hao wamekuwa wanakumbana na matatizo mengi ambayo yanadhoofisha sana maendeleo yao kielimu hivyo wakazi wa kisiwa cha Rukuba wameamua kujenga sekondari yao kisiwani humo.
Akizungumza kwenye harambee hiyo mbunge wa jimbo la Musoma vijijini Profesa Sospeter Muhongo amewashukuru wananchi wa kisiwa hicho kujitoa kuchangia ujenzi huo.
Amesema kutokana na kasi waliyoanza nayo ipo imani ya sekondari hiyo kukamilika kwa muda mfupi.
Kwa upande wao wakazi wa kisiwa cha Rukuba wamemshukuru mbunge huyo kwa kuendesha harambee kwaajili ya kuwasaidia kupata shule ya sekondari.