Home Kitaifa MUHONGO AONGOZA HARAMBEE UJENZI WA MAABARA SEKONDARI YA ETARO

MUHONGO AONGOZA HARAMBEE UJENZI WA MAABARA SEKONDARI YA ETARO

-ACHANGIA MIFUKO 100 YA SARUJI BATI 100

-ASHUHUDIA CHUMBA CHA MAABARA YA KOMPYUTA

Na Shomari Binda-Musoma

MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini Profesa Sospeter Muhongo ameongoza harsmbee ya ujenzi wa chumba cha maabara ya fizikia shule ya sekondari Etaro.

Katika harambee hiyo Muhongo amechangia mifuko 100 ya saruji kama mchango binafsi wa mbunge na bati 100 kutoka mfuko wa jimbo.

Wananchi wa Kata ya Etaro wamechangia fedha taslim shilingi 850,000 pamoja na mifuko 3 ya saruji huku wakiendelea na michango.

Akizungumza kwenye harambee hiyo Muhongo amesema dunia ya leo sayansi na wanayansi ndio wenye nafasi kubwa kwenye shughuli mbalimbali hivyo ni muhimu kuwekeza kwenye masomo ya sayansi.

Amesema kwa sasa shule hiyo ina maabara moja ya bailojia inayotumika maabara ya kemia inaendelea kujengwa na serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 30 kwaajili ya ukamilishaji ifikapo mwishoni mwa mwezi desemba mwaka huu.

Maabara ya 3 ya fizikia tayari wananchi walishaanza ujenzi wake ikiwa kwenye hatua ya kupaua na kuezeka na harambee iliyoendeshwa na mbunge Muhongo inatarajia kukamilisha.

Amesema wananchi wa Kata ya Etaro wanapaswa kupongezwa kwa jitihada zao za kuchangia sekta ya elimu hususani masomo ya sayansi.

Ndugu zangu wa Kata ya Etaro niwashuuru sana kwa jitihada zenu kwenye masuala ya kuchangia hususani kwenye ujenzi wa maabara.

Kwa kuunga mkono jitihada zenu mimi nachangia mifuko 100 ya saruji na mabati 100 kutoka mfuko wa jimbo ila tuendelee kuchanga ili tukamilishe maabara zetu“,amesema Muhongo.

Akiwa shuleni hapo mbunge Muhongo ametembelea chumba cha maabara ya kompyuta na kuona wanafunzi wakiendelea kujifunza matumizi yake.

Shule hiyo imepokea kompyuta 25 ikiwa ni msaada kutoka chuo kikuu cha Northern Illinois cha nchini Marekani ambao ni marafiki wa shule hiyo.

Wananchi wa Kata ya Etaro wamemshukuru mbunge Muhongo kwa jitihada zake za kuchangia shughuli za maendeleo ikiwemo elimu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!