Na Shomari Binda-Musoma
MBUNGE wa jimbo la Musoma vijijini,Prof.Sospeter Muhongo, amemuelezea namna alivyomfahamu aliyekuwa mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Herman Kirigini.
Akitoa salama za rambirambi wakati wa kuaga mwili wa Kirigini kuelekea Kijiji cha Muliaza wilayani Butiama kwaajili ya mazishi,amesema alikuwa mtu wa pekee katika kuwahufumia wananchi.
Amesema leo vijana asilimia kadhaa walioko makazini kwenye ogisi za serikali nabinafsi wapo ambao wamepitia mikono ya Herman Kirigini.
Muhongo amesema ni viongozi wachache ambao wanaweza kusimama na kusaidia jamii inayowazunguka kama ambavyo alifanya hivyo.
Amesema yeye kwa upande wake binafsi ameweza kusaidiwa na marehemu Herman Kirigini, wakati akiwa kiongozi kwa kumsaidia kutoa gari bandarini.
“Marehemu Herman Kirigini alikuwa kiongozi wa pekee katika kuisaidia jamii yake nasi tunapaswa kuiga mfano wake tuliobaki hai”,amesema Muhongo.
Akisoma wasifu wa marehemu,Peter Kirigini ,amesema Herman Kirigini,alizaliwa desemba 22 mwaka 1945 na katika kipindi cha uhai wake ameshika nafasi mbalimbali za uongozi.
Amesema Herman Kirigini alikuwa Waziri wa kwanza wa mifugo na baadae Waziri wa Kilimo na Mifugo na akiwa mbunge wa jimbo la Musoma vijijini.
Peter amewashukuru madaktari waliokuwa wakimuhudumia baba yao kipindi cha ugonjwa wake wa kisukari uliokuwa ukimsumbua tangu akiwa na miaka 30.
Marehemu Herman Kirigini, aliyefariki mei 23 anatarajiwa kuzikwa jesho mei 27 kijijini kwake Muriaza wilaya ya Butiama.