Waziri wa Fedha Mhe. Dk. Mwigulu Nchemba ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutowaonea huruma watu wanaokwepa Kodi bila kujali ukubwa au umaarufu wao.
Akifungua kikao cha nusu mwaka cha kutathmini utendaji kazi wa TRA kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Jijini Arusha leo tarehe 06.01.2025 Waziri wa Fedha Dk. Nchemba amesema suala la kulipa kodi ni la kila mmoja maana kodi inayokusanywa ni kwaajili ya maendeleo ya nchi.
Amesema Nchi haiwezi kujitegemea kama Kodi hailipwi kikamilifu na kuitaka TRA kutoogopa lawama kwenye masuala ya Kodi yanayohusu sheria na taratibu.
Dk. Mwigulu ameipongeza TRA kwa kuvunja rekodi ya makusanyo ya Kodi kwa Mwezi Desemba tangu kuanzishwa kwake kwa kukusanya kiasi cha Sh. Trilion 3.587 na pia kuvuka malengo ya nusu mwaka kwa kukusanya Sh. Trilion 16.528 na kueleza kuridhishwa na utendaji kazi wao.
Amesema utaratibu ulioanzishwa na Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda wa kuwafuata Walipakodi na kuwasikiliza umeongeza makusanyo bila kutumia nguvu na kuweka ukaribu baina ya TRA na Walipakodi.
Dk. Mwigulu amesema kumekuwa na mtazamo hasi juu ya TRA kukusanya Kodi na kutaka elimu iendelee kutolewa kwamba kodi inayokusanywa ni kwaajili ya maendeleo ya nchi na makusanyo yote yamekuwa yakipelekwa kwenye mfuko mkuu wa Serikali kwaajili ya kupangiwa matumizi.
“Jamii inapaswa kueleweshwa vya kutosha kuhusu masuala ya Kodi kwamba ni za kwetu sote siyo za TRA hata risiti za EFD ni za kwetu wote kwaajili ya maendeleo ya nchi hivyo mtu anayekwepa Kodi anapaswa kuwa adui wa kila mmoja wetu maana anatukwamisha” Dk. Mwigulu.
Waziri wa Fedha amesema TRA inao wajibu wa kulinda na kuboresha biashara za Walipakodi ili zikue waweze kulipa Kodi na pia Mamlaka hiyo inawajibika katika kujenga Uchumi badala ya kusubiri kukusanya Kodi.
Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda akimkaribisha Waziri wa Fedha amesema wataendelea kutoa elimu kwa Walipakodi kuhusu kulipa Kodi kwa hiari na kuwatembelea ili kusikiliza changamoto zao na kuzitatua.
Aidha amesema kwa eneo la Elimu, wataanza kuwatumia Wanamichezo, Wasanii na Viongozi wa Dini zote kutoa Elimu ya Kodi kwa jamii ili Walipakodi watambue kwamba ni wajibu na jukumu lao kulipa Kodi.
Kamishna Mkuu Mwenda amesema TRA imekuwa ikiboresha utendaji kazi wake kwa kutumia mifumo ili kupunguza watumishi wa Mamlaka hiyo kukutana na Walipakodi ambapo January 20 mwaka huu mfumo wa TANCIS ulioboreshwa utaanza kutumika.
Amesema mfumo huo ambao utafanya kazi Bandarini, mipakani na katika Viwanja vya Ndege utaleta tija ya makusanyo na kuboresha utendaji kazi wa TRA na Wakala wa Forodha.
Katika hatua nyingine Kamishna Mkuu Mwenda amesema mahusiano mazuri waliyoyaweka baina ya TRA na Walipakodi pamoja na vyama vya wafanyakazi ndiyo yamesaidia kuongeza ukusanyaji wa Kodi.
Amesema wanapokwenda kwenye nusu ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025 wataendelea kupambana na wakwepa kodi wa aina zote wakiwemo wanaotoa Makadirio yasiyokuwa sahihi, wasiotoa risiti na wanaotoa risiti bandia pamoja na wanaoingiza bidhaa za Magendo.
Mwisho