Home Kitaifa MSIJIFICHE MAJUMBANI, TRAKOMA INATIBIKA KWA UPASUAJI KUEPUSHA UPOFU – KABALIKA.

MSIJIFICHE MAJUMBANI, TRAKOMA INATIBIKA KWA UPASUAJI KUEPUSHA UPOFU – KABALIKA.

NA.Catherine Sungura – DAR ES SALAAM

Watu walioathiriwa na ugonjwa wa vikope {trakoma} wamehimizwa wasijifiche na kusalia majumbani, wakiogopa kujitokeza kufuata matibabu katika vituo vya kutolea huduma afya kwa sababu ugonjwa huo unatibika kwa njia ya upasuaji.

Rai hiyo imetolewa hivi karibuni Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika lisilo la kiserikali la SightSavers Tanzania, Godwin Kabalika alipozungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano ulioandaliwa na Wizara ya Afya uliojikita kujadili kuhusu magonjwa yasiyopewa kipaumbele ukiwamo huo wa Trakoma.

Kabalika alisema mgonjwa anapofanyiwa upasuaji hatua hiyo humuondoa katika uwezekano wa kupata upofu wa kudumu unaoweza kujitokeza kutokana na athari za ugonjwa huo.

“Sisi kama shirika letu tumeweza kuisaidia Wizara ya Afya katika mikoa mitano Ruvuma, Lindi, Morogoro, Singida, na Manyara na mafanikio makubwa tuliyoona ni kwamba tumeweza kusaidia watu mbalimbali ambao waligundulika wana ugonjwa wa vikope {Trakoma}.

Aliongeza “Kama isingekuwa kuwasaidia kwa haraka/mapema ingeweza kusababisha upofu, tunajivunia tumeweza kusaidia, kuwafanyia upasuaji wagonjwa wengi ambao matokeo yake wanaweza kuona.

Alisema ikiwa si hivyo wangekuwa vipofu kabisa na kuongeza “Kikubwa tunajivunia wanaweza kufanya shughuli zao vizuri kama binadamu wengine na wanaweza kuchangia kwenye maendeleo, kujikwamua kwenye familia kwenye jamii.

“Kwa ujumla kwa nchi nzima wamekuwa sehemu ya kuifikisha Tanzania kwenye maazimio yake ya kiuchumi,” alisema.

Alisema bado zipo imani potofu kwenye jamii kuhusu ugonjwa na kwamba Shirika hilo kupitia watoa huduma za afya ngazi ya jamii {CHWs} limekuwa likiendelea kuelimisha jamii.

“CHWs hao wanapita kwenye jamii, nyumba kwa nyuma wanafanya mikutano na wanawaeleza wananchi ili kutoa ile dhana potofu kwamba ni wa kurithi, wagonjwa wengine wanafichwa.

“… kunakuwa na hisia mbalimbali na kuamini vitu ambavyo si vya kweli,” alisisitiza Kabalika.

Alisema kutokana na uelimishaji unaofanyika kwenye jamii wameweza kuona mwitikio mkubwa kwa watu kuendelea kujitokeza kupata matibabu.

“Wengi wamekuwa wakija au tunawafuata na kufanya upasuaji, tunaendelea kutoa hiyo elimu, tunawatumia hata wale waliofanyiwa upasuaji kwamba hili jambo linawezekana ukifanyiwa upasuaji unarudi kwenye jamii bila tatizo lolote lile.

“Tunao watu Ruvuma, Morogoro, Manyara watoto wametibiwa na hata watu wazima na wamerudi kwenye shughuli zao, ni ugonjwa unaotibika si kwa gharama kubwa na hauna changamoto wowote.

“Wito wangu kama kuna jamii ina wagonjwa wa namna hiyo mara moja wasisite kutoa taarifa kwa kufika kwenye kituo chochote kinachotoa huduma za afya au wadau wowote wanaosaidia kutoa huduma.

Mkurugenzi huyo alisema SightSavers Tanzania limekuwa likifanya shughuli zake nchini tangu miaka ya 70 kwa ushirikiano wa karibu na Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kujikita kufanya elimu jumuishi ya masuala ya afya ya macho na ya watu wenye ulemavu.

Kuhusu mkutano huo wa kujadili magonjwa yasiyopewa kipaumbele {negretaded tropical diseases} ni wa muhimu kwani ulikutanisha wadau wengi wanaoshiriki katika mapambano dhidi ya magonjwa hayo.

“Sisi kama wadau tumeongea changamoto kwa pamoja zinazohusiana na magonjwa haya, lakini pia zaidi umewezesha wadau wote ambao wanasaidia katika mapambano dhidi ya magonjwa haya kuweza kupanga kwa pamoja.

“Yaani tunajadili changamoto mbalimbali, tunajadili maendeleo tuliyofanya au hatua zilizofanyika mpaka sasa zenye kuweza kusaidia,” alisema.

Aliongeza “Kimsingi tumeweza kujadili nini tufanye pamoja, tuweze kupanga pamoja kuhakikisha tunatokomeza magonjwa haya yasiyopewa kipaumbele nchini Tanzania.

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!