Home Kitaifa Mshindi kwa kilimo cha Pamba 2022 aahidi kupata kilo 2000 kwa hekari

Mshindi kwa kilimo cha Pamba 2022 aahidi kupata kilo 2000 kwa hekari

Na Neema Kandoro, Nyang’wale

MKULIMA mshindi kitaifa kwa kilimo cha pamba mwaka 2020/21 kutoka Kijiji cha Kaboha wilayani Nyang’wale Mkoani Geita amewataka wakulima kuongeza juhudi wapate kilo 2000 kwa ekari kukabili kushuka kwa bei ya zao hilo duniani.

Mshashi Kalulu aliiambia Mzawa Blogs Jana kijijini hapo kuwa kutokana na ushauri wa Maofisa ugani wanaotoa kwao wa namna ya uwekaji mbolea ya samadi kwenye mashamba kupanda kwa sentimita 30 kwa 60 wanakusudia kupata kilo 2000 kwa ekari msimu huu.

Kalulu ambaye aliibuka kidedea kwa kuwa mkulima bora na kuzawadiwa trekta amekuwa akifikiwa na wakulima wa pamba toka sehemu mbalimbali kupata maarifa ya kuinua mavuno yao kwenye mashamba yao.

“Wakulima wa pamba kijijini hapa na maeneo jirani hunifikia wakati wa kilimo na kuniomba ushauri waweze kufanya vizuri hivyo nawaambia walime mashamba madogo waweze kuyatunza vizuri” alisema Kalulu.

Alisema kipindi anapata ushindi huo mwaka 2021 alipata kilo 4820 kwa ekari nne, hivyo msimu uliofuata 2022 alilima ekari mbili na kupata kilo 3600 na sasa atalima ekari mbili apate kilo 4000.

Wakulima wanaofika na kunitaka ushauri tumekubaliana msimu huu tupate kilo 2000 kwa ekari moja kwani endapo tutaongeza mavuno hatuwezi kuathirika endapo kutatokea mtikisiko wa bei.

Mkulima wa Kijiji cha Kamashi Kata ya Bulela wilayani hapo Hoja Lunilija alisema kuwa amesomba mbolea ya samadi ya kutosha shambani kwake ili aweze kupata mavuno ya kilo 2000 kwa ekari moja msimu huu.

Naye mkulima wa kijiji cha Kaboha Manugwa Mathias alisema ameacha kulima kwa mazoea kilimo cha pamba kwa sasa anazingatia masharti ya kitaalamu hivyo wamekubaliana wapate kilo 2000 katika eneo la ekari moja.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!