Home Michezo MSHIKEMSHIKE MASHINDANO YA UMITASHUMTA TARAFA YA MUMBUGA YAZIDI KUUNGURUMA.

MSHIKEMSHIKE MASHINDANO YA UMITASHUMTA TARAFA YA MUMBUGA YAZIDI KUUNGURUMA.

#Walimu makocha watoana jasho kulinda heshima ya kata zao

#Hamasa yazidi kupamba moto huku timu nyingine zikipoteza matumaini

#Refa wa Mchezo Mwl. Shendu Maduhu aonesha ufundi uwanjani; Viongozi wa timu wabaini mapungufu kwa wachezaji wao

Ligi ya UMITASHUMTA ngazi ya tarafa ya Mumbuga iliendelea tena jana April 25, 2024 katika viwanja mbalimbali vilivyopo katika tarafa ya Mumbuga ili kuunda timu imara itakayoshindanishwa na tarafa zingine kuunda timu bora ya UMITASHUMTA ngazi ya Wilaya ya Ukerewe.

Mchezo wa kwanza ulizikutanisha timu kutoka kundi A, ambapo timu kutoka kata ya Nkilizya ilikutana na timu kutoka kata ya Namagondo katika uwanja wa Bukongo, muamuzi katika dakika zote 90 za mchezo alikuwa ni Mwl. Shendu Maduhu kutoka Shule ya Msingi Bukongo.

Mpaka kipyenga cha mwisho kinapulizwa timu kutoka kata ya Namagondo chini ya kocha wao Mwl. Wolta Njuu iliibuka na ushindi wa goli 1 kwa 0, goli likifungwa na kiungo mshambuliaji Derick Zelemani katika dakika ya 26 na hivyo kuondoka na alama zote tatu.

Mchezo mwingine wa kundi A, ulizikutanisha timu kutoka kata ya Bukongo na kata ya Nansio katika uwanja wa shule ya msingi Nkilizya ambapo timu kutoka kata ya Bukongo ilifanikiwa kuibuka na ushindi mnono wa magoli 3-1 dhidi ya timu ya kata Nansio hali iliyopelekea kufifisha matumaini ya Nansio watoto wa mjini kuendelea katika hatua inayofuata.

Aidha, katika kundi B ilichezwa michezo mingine miwili ya mpira wa miguu ambapo mchezo wa kwanza ulizikutanisha timu ya kata ya Ngoma na kata ya Kagera katika uwanja wa shule ya msingi Ukerewe EM, mpaka mchezo unakamilika timu ya kata ya Ngoma waliibuka na ushindi wa magoli 3-2 dhidi ya timu kutoka kata ya Kagera.

Aidha, katika mashindano hayo, mchezo mwingine kutoka kundi B ulichezwa katika uwanja wa Shule ya Msingi Kakerege ambapo uliozikutanisha timu majirani kati ya Kakerege Vs Nakatunguru, mchezo ambao uliosimamiwa na muamuzi Elias Pantaleo ambapo mchezo timu hizo zilitoka sare ya goli 1-1.

Kwa upande wa mpira wa Pete kundi A timu kutoka kata ya Nkilizya iliangukia pua kwa kunyukwa magori 29 kwa 5 dhidi ya timu kutoka kata ya Namagondo na timu kutoka kata ya Nansio iliwaadhibu timu ya kata ya Bukongo magori 16 kwa 8.

Katika kundi B timu ya kata ya Ngoma iliwafunga magori 32 kwa 2 dhidi ya timu kutoka kata ya Kagera na timu kutoka kata ya Nakatunguru ilinyukwa magori 28 dhidi ya timu kutoka kata ya Kakerege iliyoambulia magori 2 mpaka mchezo kukamilika.

Michezo mingine itaendelea kurindima tena dimbani April 29, 2024 kwa kuzikutanisha timu kutoka kundi B ambapo timu ya kata ya Bukanda itavaana vikali na timu kutoka kata ya Kagera na timu kutoka kata ya Ngoma itavaana na timu kutoka kata ya Nakatunguru kwa mpira wa miguu na pete.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!