Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Bw. Christopher Mramba amewashauri wafanyabiashara kuzingatia sheria na kuendelea kujenga utamaduni wakuzingatia masharti ya ubora wa bidhaa zinazoingizwa nchini kwa kuwa Serikali haitaacha soko la Tanzania liwe dampo la kuweka bidhaa zisizo na ubora.
Bwana Mramba amayasema hayo Akizungumza na waandishi wa habari Septemba 30 , 2022 katika ofisi za Shieika la Viwango Tanzania (TBS) Jijini Dar es Salaam wakati wa uchunguzi wa mabati yaliyoingizwa nchini na kampuni ya uagizaji na usambazaji wa mabati nchini URHOME Company Limited
“Tutaendelea kushirikiana na vyombo vya Serikali kufuatilia bidhaa ambazo zimeingia sokoni kinyume na sheria na kuchukua hatua stahiki za kisheria” Amesema Bw. Mramba.
Aidha, Bw. Mramba ametoa wito kwa wafanyabiashara wote nchini kuzingatia uaminifu na matumizi mazuri ya fursa zinazotolewa na Serikali za kuweka mazingira wezeshi ya biashara ikiwemo hii fursa ya kutoa kibali cha masharti maalumu ya kutoa mzigo bandarini ili bandari yetu iendelee kuwa na ufanisi unaotakiwa na pasiwe na msongamano ili biashara nyingine ziweze kufanyika.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Bw. David Ndibalema amewahimiza wafanyabiashara na waingizaji wa bidhaa kutumia vizuri vibali vya masharti kwa kuhakikisha wanazingatia yale masharti ambayo yamewekwa wakati wa kutoa vibali hivyonikiwemo kutokusambaza, kuuza, au kutumia njia yoyote ile kutoa mzigo kabla ya uchunguzi kukamilika.
Aidha, TBS imeiandikia barua kampuni hiyo ya uagizaji na usambazaji wa mabati nchini URHOME Company Limited kuhakikisha ndani ya siku tatu wawe wametoa taarifa ya mabati 2176 kati 125280 yapo wapi baada ya kufanyiwa ukaguzi na kugundulika hayajakidhi viwango.
Naye, Meneja wa uthibiti wa Shehena zinazoingia na kutoka nchini Mhandisi Saidi Mkwawa amesema Kampuni hiyo baada ya kuingiza nchini mabati hayo, TBS ilichukua sampuli na kuzipeleka kwenye maabara ya Shirika ili kubaini kama zimeweza kukidhi viwango stahiki kwa mujibu wa sheria .
Pamoja na hayo Mhandisi Mkwawa amesema watahakikisha mabati yote yanapatikana na zoezi la uteketezaji litaendelea sambamba na mengine.