Mradi wa maji wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Simiyu maandalizi yake yameshika kasi ambapo hivi sasa kazi ya kuhamisha maeneo ya maziko ili kupisha eneo la bomba kuu la maji litakaloanzia ziwa Victoria inaendelea.
Mratibu wa mradi huo Mhandisi Mwajuma Waziri wa Wizara ya Maji amesema kazi hiyo ya kutoa nafasi kwa kuhamisha maeneo ya maziko ni shirikishi na inawahusisha ndugu wa familia pamoja na viongozi wa Serikali za Mitaa katika maeneo yanayohusika.
Aidha, Mhandisi Waziri amesema jumla ya makaburi 78 yanatarajia kuhamishwa, na hadi leo Juni 20 zaidi ya makaburi 22 yamechimbwa na kuhamishwa mabaki kwa kushirikiana na familia husika, na viongozi wa Serikali za Mitaa, na kuyazika katika maeneo mapya yaliyoanishwa na familia husika, nje ya eneo la bomba kuu.
“Kila familia iliyoadhirika na zoezi hili inapewa asante na serikali, na endapo mabaki hayatapatikana kwasababu yoyote, ikiwamo kukosea alama za mahali lilipo kaburi, wakati wa ujenzi mabaki yakipatikana basi familia husika itapewa stahiki kama ilivyopangwa na Serikali”
Mhandisi Waziri amewaambia wakazi wa Itilima wakati wa kuhamisha mabaki yaliyopatikana katika moja ya kaburi, na kuongeza zoezi lote linagharamiwa na Serikali.
Ameongeza kila kaburi litakalochimbwa kutakuwa timu ya wataalamu wa afya watakagua mabaki ili kujiridhisha endapo ni mabaki ya binadamu, ili kuweka uwajibikaji kwa jamii na malipo. Mradi wa maji wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi Simiyu ni moja ya mradi wa maji utakaoleta mapinduzi makubwa kwa kuwahudumia wananchi, mifugo na kuendeleza masuala ya kilimo.