
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (MNEC) kutoka Mkoa wa Geita, Evarist Gerves, amekemea vikali tabia ya baadhi ya vijana wa chama hicho kuwatusi viongozi na watu waliotangaza nia ya kugombea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu kupitia magroup mbalimbali ya WhatsApp. Ametaja tabia hiyo kuwa kinyume cha maadili ya CCM.
Evarist alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kata ya Lulembela, Wilaya ya Mbogwe, katika ziara yake iliyoeleza sababu za Mkutano Mkuu wa CCM kumpitisha Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa urais katika uchaguzi mkuu ujao.
Amesema kumekuwepo na baadhi ya watu, wakiwemo viongozi, wanaowaunganisha vijana kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya mkoa wa Geita kwa lengo la kuwaandaa kuwatukana viongozi pamoja na wale wanaoonyesha dhamira ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi. Ameonya vikali tabia hiyo na kuwataka vijana wa CCM kuzingatia maadili ya chama.
Evarist amesisitiza kuwa CCM ni chama chenye misingi ya mshikamano na heshima, hivyo hakuna nafasi kwa tabia za matusi, kejeli, na uchochezi ndani ya chama.
“Tunapaswa kushindana kwa hoja, si kwa matusi. Wale wanaotaka uongozi wakati ukifika ni ruksa kabisa wao kujitokeze hadharani, waeleze sera zao badala ya kushiriki katika matusi kupitia mitandao ya kijamii,” alisema.
Aidha, amewataka vijana kutumia mitandao ya kijamii kwa manufaa ya chama na jamii kwa ujumla, huku akisisitiza umuhimu wa kuenzi umoja na mshikamano ndani ya CCM kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.