Mkuu wa Wilaya ya Tanga Mheshimiwa James Kaji amewaalika wakazi wa Mkoa wa Tanga kutembelea banda la Chuo Kikuu Mzumbe katika maadhimisho ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayoendelea kwenye Viwanja vya Shule ya Popatlal Jijini Tanga ili kupata uelewa wa kozi na huduma nyinginezo zinazotolewa na Chuo hicho kwenye maonesho hayo.
Mheshimiwa Kaji ambaye pia ni mhitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe amesema kuwa Tanga ni miongoni mwa Mikoa ambayo haina vyuo vikuu hasa vya serikali na hivyo maonesho hayo ni fursa adhimu kwa wananchi kutembelea na hasa kutembelea banda la Chuo Kikuu Mzumbe ambacho tayari kimeshapata eneo Wilayani Mkinga kwa ajili ya kujenga Chuo Kikuu Ndaki ya Tanga kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) na kuanza huduma mkoani Tanga.
Aidha Mheshimiwa Kaji amekipongeza Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuanza taratibu za kufungua Kampasi katika wilaya ya Mkinga Jijini Tanga na kushauri kutokana na uhitaji mkubwa wa elimu ya juu mkoani humo Chuo Kikuu Mzumbe kuanza kutoa mafunzo kwenye majengo ya kupanga hadi ujenzi wa majengo yao utakapokamilika kwani wananchi wengi hasa watumishi wamekuwa wakipata changamoto ya kujiendeleza kutokana na kutokuwepo kwa vyuo vikuu mkoani Tanga huku wengine wakikosa likizo za masomo ya muda mrefu kwa Waajiri wao
“Nachukua fursa hii kushauri uongozi wa Chuo kuangalia namna ya kuanza kutoa huduma kwa kutafuta majengo ya kukodi kwani katika Jiji letu kuna uhitaji sana kwa wanaotaka kujiunga na Elimu ya Juu” alisisitiza Mheshimiwa Kaji.
Amewapongeza washiriki wa maonesho hayo katika banda la chuo kikuu Mzumbe kwani wamekuwa wakitoa maelezo vizuri kwa wageni na pia muonekano wabanda lao ni mzuri sana
Chuo Kikuu Mzumbe ni miongozi wa vyuo vya elimu ya juu vinavyoshiriki katika maoneosho ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yaliyoanza Mei 25 hadi 31, 2024 katika viwanja vya Shule ya Sekondari Popatlal ambapo Chuo Kikuu Mzumbe kinaonyesha mambo mbalimbali ikiwemo Ushauri wa kujiunga, Ufafanuzi wa kozi zinazotolewa, Udahili wa papo kwa papo.
Huduma zingine zinazotolewa kwenye banda hilo ni Huduma za Maktaba, Kuonesha bunifu na huduma za kijasiriamali, kuonesha utekelezaji na matokeo ya tafiti na miradi inayotekelezwa na Chuo pamoja na kuwakaribisha na kuwasajili wahitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe (Alumni).