Ashrack Miraji Mzawa Online Media
Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, amewataka wanafunzi wa shule za sekondari wilayani humo kujiepusha na vitendo vinavyoashiria mmomonyoko wa maadili ikiwemo ushoga, usagaji, mapenzi kabla ya umri pamoja na utoro, akisisitiza kuwa mienendo hiyo inaweza kuhatarisha mustakabali wao na kupelekea kukatisha ndoto zao za kielimu.
Akizungumza na wanafunzi wa baadhi ya shule akiwa kwenye ziara ya kufuatilia hali ya mahudhurio ya wanafunzi kwa mwaka 2025, Mhe. Kasilda alisema vitendo vya mmomonyoko wa maadili vinakwamisha juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha elimu nchini.
“Mimi, kama Mkuu wa Wilaya, nataka ninyi mtimize ndoto zenu. Ni marufuku kujihusisha na vitendo vyovyote vya mmomonyoko wa maadili vikiwemo kujihusisha na mapenzi, usagaji, ushoga pia utoro kwa kuwa vitendo hivyo vinarudisha nyuma jitihada za serikali katika kuinua sekta ya elimu,” alisisitiza Mhe. Kasilda.
Aidha, aliwasihi wanafunzi hao kuwa makini na maudhui wanayopokea kutoka kwenye mitandao ya kijamii, akibainisha kuwa baadhi ya mambo yanayopatikana huko yanaweza kuathiri mwenendo wao wa masomo na tabia zao kwa ujumla.
“Niwaombe sana wanangu, kama kweli tunataka kuja kulisaidia Taifa hili tuachane na hivi vitendo, Mambo mengi yapo kwenye mitandao, lakini sio kila unachokiona kwenye mtandao ni cha kuiga mengine yatawaharibu na yatasababisha mpoteze malengo yenu” Alisema Mhe. Kasilda.
Kwa upande wake, Afisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Same alisema wameanzisha mkakati wa kufuatilia wanafunzi watoro kwa kushirikiana na wazazi wao, huku hatua za kisheria zikichukuliwa pale inapobidi ili kuhakikisha kila mtoto anapata haki yake ya msingi ya elimu.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuhakikisha kila mwanafunzi anapata elimu bora na kuimarisha usimamizi wa shule kwa ustawi wa vijana na maendeleo ya taifa kwa ujumla.