Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amefungua Mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa unaoshirikisha wadau wa Demokrasia ya Vyama vingi vya Siasa kujadili Miswaada ya Sheria za Uchaguzi na Mswaada wa Sheria za Vyama Vya Siasa Nchini.
Akizungumza kwenye Mkutano huo, Mhe. Othamn amesisitiza juu ya uwasilishwaji , Upekeaji na Ufanyiaji kazi wa maoni ya kila mdau na si kugeuza Mkutano huo kuwa muhuri wa kuwasilisha mawazo ya Watu wachache au Misimamo ya Kitaasisi.
“Jambo hili la leo ni adhimu kwa manufaa ya Taifa letu katika kuimarisha Demokrasia, Nalipongeza Baraza la Vyama Vya Siasa Nchini kwa ushirikiano wenu ambao kwa pamoja tumeweza kuitisha Mkutano huu muhimu“
“Kuwashirikisha wadau mbalimbali katika jambo lenye maslahi mapana ya Taifa letu wapo watu wanachukulia kama jambo tu la kawaida, lakini kama Watanzania lazima tuthamini utamaduni huu kwamba umejengeka kutoka na historia yetu, umahiri wa Viongozi wetu waliotangulia na waliopo, Pia kwa mchango mkubwa wa kila mmoja wetu kama Viongozi na Kama Wananchi, Tuuthamini utamaduni huu“
“Ushahidi wa utamaduni wa hiki tunachokifanya ni taswira iliyopo mbele yetu ambapo japokuwa ni wa Baraza la Vyama vya Siasa lakini washiriki wake nimeambiwa na nimeona hapa ni zaidi ya Wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa kwani wameshirikishwa wadau mbalimbali katika makundi yote ya kijamii, hili ni jambo jema sana na hakika tunamuunga mkono Rais Mhe. Dkt. Samia ambaye amekuwa akitoa wito katika kukutana huku“
“Utaratibu wa kukutana na kuzungumza unatoa fursa kwa Watanzania kupitia Taasisi mbalimbali zinavyowawakilishwa na kwasababu hiyo nawasihi mkutano huu uache alama ya majadiliano mema, uwe mkutano wa utajiri wa mawazo ya washiriki na sio mkutano wa mapambio na kutimiza tu utaratibu na kusema wadau wameshirikishwa, tuepuke kugeuza kuwa muhuri wa kuwasilisha mawazo ya watu wachache au msimamo wa kitaasisi“
“Tukumbuke Desemba 2021 Baraza hili lilifanya Mkutano wake Jijini Dodoma ulipelekea kuundwa kwa kikosi kazi cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutazama hali ya Demokrasia nchini kwetu, Mwezi Aprili 2022 kituo cha Demokrasia Tanzania kikafanya mkutano Dodoma na kutoa mapendekezo mahususi ya Kikosi kazi kuhusu Sheria zetu za Uchaguzi na Vyama Vya Siasa na Septemba 2022 kikosi kazi kikakabidhi taarifa rasmi kwa Mhe. Rais na Januari 2023 Rais Samia akaondoa zuio la mikutano ya hadhara ya Vyama vya siasa na Novemba 10, 2023 Miswaada tunayoikusudia kuijadili hapa iliwasilishwa na kusomwa kwa mara ya kwanza Bungeni”
Mkutano huu unafanyika katika kituo cha Kimataifa cha Mikutano JNICC Jijini Dar es salaam.
🗓️ Leo 03 Januari, 2024
Kauli Mbiu:
” TOA MAONI YAKO KUIMARISHA DEMOKRASIA “